Header Ads

uteuzi wa watu 39 kushika nyadhifa serikalini, ikiwemo wenyeviti wa bodi



IKULU imefanya uteuzi wa watu 39 kushika nyadhifa serikalini, ikiwemo wenyeviti wa bodi za taasisi za serikali, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na makatibu tawala.
Katika mchanganuo huo, walioteuliwa kuwa wenyeviti wa bodi ni saba, wakuu wa wilaya wawili, wakurugenzi wa halmashauri watatu na makatibu tawala 27.
Wenyeviti wa bodi Katika uteuzi wake alioufanya Jumamosi, Rais John Magufuli aliwateua wenyeviti saba wa bodi za taasisi za Serikali, Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Tanzania (NEEC) na Mjumbe wa Baraza la Taifa la Biashara. Katika uteuzi huo, miongoni mwa walioteuliwa wapo wahadhiri watatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza hayo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ali Mufuruki ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira.
Mufuruki ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni za Infotech Investment na Mwenyekiti wa Taasisi ya Afrika inayojihusisha na uendelezaji wa vipaji vya uongozi katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Rais pia amemteua Christopher Chiza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade). Chiza amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika uongozi nchini, ikiwemo Waziri wa Uwezeshaji na Uwekezaji na Naibu Waziri Kilimo, Chakula na Ushirika wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Katika uteuzi huo, Chiza anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Sabetha Mwambenja ambaye amemaliza muda wake. Mwingine aliyeteuliwa jana na Rais Magufuli ni Peter Maduki.
Maduki anakuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Idrissa Mshoro aliyemaliza muda wake. Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA)imepata mwenyekiti mpya ambaye ni Dk Yamungu Kayandabila.
Dk Kayandabila ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Peter Ilomo aliyemaliza muda wake.
Wengine walioteuliwa na nafasi zao kwenye mabano ni Profesa Godwin Mjema (Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Huduma za Fedha na Mikopo-UTT-MFI).
Prof. Daniel Mjema ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Fadhili Mbaga ambaye amemaliza muda wake.
Rais pia amemteua Kapteni Ernest Bupamba kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Bahari (DMI). Bupamba ni Mwendesha Meli Mkuu katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Mwingine aliyeteuliwa ni Dk Aloyce Hepelwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Miradi ya Maendeleo ya Miundombinu (UTT-PID).
Dk Hepewa ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia Rais Magufuli amemteua Dk John Jingu kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi Tanzania. Dk Jingu ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Pia amemteua Dk Rashid Tamatama ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI).
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi inayojihusisha na huduma za ushauri wa ubora na mafunzo (Service Limited) katika ofisi zake za Dar es Salaam Zuhura Muro yeye aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Taifa la Biashara). Wateule hao uteuzi wao umeanza juzi Jumamosi.

No comments