Header Ads

RAIS John Magufuli amefichua siri


Image result for picha ya magufuli


RAIS John Magufuli amefichua siri iliyosababisha asafiri hadi mjini Singida kwenda kusali ibada ya Krismasi katika Kanisa la Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Katoliki la Singida.
Amesema kilichosabisha yeye kwenda kusali kwenye kanisa hilo ni kwa kuwa alikabidhiwa Rozari na mtawa mmoja wa kike (sista) ambaye hata hivyo hamkumbuki sura wala jina wakati akiwa katika kampeni ya Urais mwaka 2015.
"Aliniambia chukua rozari hii ikusaidie katika kampeni yako. Naamini nafasi hii nimeipata kutokana na rozari hiyo. Kwa niaba yenu, napenda kumshukuru huyo sista ingawa simkumbuki".
Alipopewa fursa ya kuzungumza kwenye ibada hiyo, Rais Magufuli alirudia wito wake wa kuwahimiza Watanzania kote nchini bila kujali itikadi za vyama, kuhubiri kwa nguvu zao zote upendo na umoja ili nchi iendelee kuwa na amani na utulivu kama Yesu Kristo ambaye hakuwa CCM wala Chadema.
"Yesu hakuwa Chadema wala CCM bali alikuwa wa watu wote. Alijishusha ili aweze kututumikia. Tunapoadhimisha Sikukuu hii tukumbuke kuhubiri aliyofanya yeye..... upendo, umoja, kusameheana na wala tusibaguane" alisema. Aidha, alirejea umuhimu wa Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili nchi iweze kufikia maendeleo ya kweli katika kutekeleza azma ya Serikali kuwa na nchi ya Viwanda.
"Tuchape kazi kwa sababu hakuna kitu cha bure na maendeleo ya kweli huja kwa kufanya kazi," alisema huku akitoa angalizo kwa wakulima wa mkoa wa Singida juu ya umuhimu wa kutumia mvua chache kwa kupanda mazao yanayostahili ukame.
"Serikali tupo pamoja na ninyi katika kujenga na kuimarisha viwanda. Singida mna kiwanda kikubwa cha kukamua alizeti, lakini mnashindwa kukitosheleza kwa kuwa hakuna alizeti ya kutosha......limeni alizeti nyingi pamoja na mazao mengine," alisema Rais Magufuli.
Awali Askofu wa Jimbo hilo, Mhashamu Edward Mapunda alitoa mwito kwa Watanzania kuheshimu ulimwengu na mazingira yake.
Askofu Mapunda alisema kuwa shughuli za kibinadamu zimekuwa zikiharibu kwa kiasi kikubwa mazingira ya nchi yetu, ikiwa ni pamoja na vyanzo vyote vya maji.
"Sasa hatupati mvua za kutosha kwa sababu ya uharibifu wa mazingira.....tunalialia kwa ajili ya uovu wetu. Lakini mbaya zaidi tunaendelea kuzaa. Hao watoto watapata wapi hewa safi? " alihoji na kuwataka wananchi kupanda miti kwa wingi.
"Pandeni miti kila mnaposherehekea tukio au sikukuu yoyote.... Ukichumbia, panda mti. Ukioa au kuolewa panda mti na ukizaa panda mti siku hiyo ili mtoto akue nao," alisema Askofu Mapunda kwa mzaha lakini akifikisha ujumbe kwa uhakika.
Alisema kuwa kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaendana na maana halisi ya Krismasi huku akisema hakuna haja ya kusherehekea wakati tunaendelea kuharibu alichoumba Mungu.

No comments