MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais John Magufuli ametetea uamuzi wake
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais John Magufuli ametetea uamuzi wake wa kufanya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NC) ya chama hicho Ikulu jijini Dar es Salaam, akisema bila wanaCCM asingekuwapo hapo.
Aidha, amesema Ikulu ni ya Watanzania wote na kwamba kama kuna chama kingine cha siasa kinataka kufanya mkutano wake hapo kinakubaliwa, lakini lazima ajenda zao zifahamike na ifahamike wanazungumza nini.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya chama hicho, NEC ya CCM imekutana katika Ikulu ya Dar es Salaam, na kwa mujibu wa Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, mara nyingi kwa kawaida vikao vya Kamati Kuu (CC) ndio hufanyika Ikulu.
Akifungua kikao hicho jana Ikulu, Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa, Rais Magufuli alisema hiyo haitakuwa mara ya kwanza kufanyia vikao vya NEC Ikulu kwa sababu bila wanaCCM asingekuwapo Ikulu.
“Ninawakaribisha sana hapa Ikulu, hapa ni kwenu, bila ninyi mimi nisingekuwapo. Sioni aibu kuwakaribisha wanaCCM kuja hapa,” alisema Dk Magufuli na kushangiliwa na wajumbe 355 wa NEC waliohudhuria kikao cha jana ambacho ni cha kwanza kwake tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa Taifa, Julai mwaka huu mjini Dodoma.
Dk Magufuli akionekana kujibu hoja za baadhi ya wanasiasa wa upinzani waliohoji hatua yake ya kufanyika kikao hicho Ikulu, aliongeza, “Hapa ni kwa Watanzania wote.” “Wanakuja wageni kutoka nje, nimewakaribisha wanamuziki, hivyo sioni ajabu kufanyizia mkutano hapa Ikulu…si kwa mwanaCCM mwenzenu. Mbona mawaziri ninakutana nao hapa,” alifafanua Dk Magufuli.
“Vyama vingine pia wanakaribishwa kuja kutumia Ikulu, waombe tu utaatibu unajulikana, ajenda zao ni lazima zifahamike na tujue wanachozungumza. Hapa ni pa Watanzania wote.” Kama vile hiyo haitoshi, Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alisema hiyo haitakuwa mara ya mwisho kwa kikao hicho kufanyika Ikulu. “Hii haitakuwa mara ya mwisho kufanyizia vikao hapa Ikulu, tutakapoamua kufanya vikao hapa hakuna atakayetupangia tufanyie wapi mkutano,” alibainisha Dk Magufuli huku akishangiliwa na wajumbe hao wa NEC.
Kwa kawaida, kwa jijini Dar es Salaam, vikao vya Kamati Kuu vimekuwa vikifanyika ofisi ndogo za CCM Mtaa wa Lumumba au Ikulu, na haijawahi kufanyika kwa kikao cha NEC Ikulu, kama alivyothibitisha Katibu Mkuu Kinana wakati akitoa taarifa za kikao hicho kabla ya kumkaribisha mwenyekiti wake.
“Watu wengi wana hamu kubwa sana na kikao hiki. Kwanza, ni kikao chako cha kwanza tangu uchaguliwe kuwa Mwenyekiti wetu kule Dodoma Julai mwaka huu. Ni mkutano wa kihistoria. Ni NEC yako ya kwanza,” alisema Kinana na kuongeza: “Kamati Kuu nyingi zimekuwa zikifanyika Ikulu, lakini sikumbuki kama NEC imewahi kukutana Ikulu. Hii ni NEC ya kwanza kukutana Ikulu, sikumbuki kwani miaka ile ya sitini (wakati wa Mwalimu Nyerere) nilikuwa shuleni.”
Alifafanua kuwa kikao hicho ni cha kihistoria kwa sababu kinafanyika wakati CCM ikielekea katika maadhimisho ya miaka 40 ya kuzaliwa kwake mwakani, miaka 55 tangu Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) na zaidi ya miaka 50 baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, miaka 25 baada ya mfumo wa vyama vingine na karibu miaka 30 baada ya mageuzi ya kiuchumi nchini.
Kwa mujibu wa Kinana, kikao cha jana kilihudhuriwa na wajumbe 355 sawa na asilimia 96.1 ya wajumbe wote 388, huku wajumbe 19 wakiwa hawapo kwa sababu mbalimbali.
Post a Comment