mwanafunzi wa kike kutozwa 200,000
MKUU wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe ameagiza kukamatwa na
kufunguliwa mashitaka Mwenyekiti wa Baraza la usuluhishi Kata ya Rungwa
wilayani Manyoni, kwa tuhuma za kumtoza faini ya Sh 200,000 mwanafunzi
wa kike anayedaiwa kujihusisha na vitendo vya ngono.
Mwenyekiti huyo, Zuberi Manjemi anadaiwa kumtoza faini hiyo
mwanafunzi wa darasa la nne kisha kumwachia bila adhabu yoyote kijana
aliyedhaniwa kuwa ni mpenzi wa binti huyo, hali iliyozua hasira ya
wazazi wa binti huyo na kuamua kutoa malalamiko yao kwenye mkutano wa
hadhara.
Katika utetezi wake, Mwenyekiti huyo alidai kuwa aliamua kumtoza
faini binti huyo pekee baada ya kukiri kupokea simu ya mkononi kutoka
kwa mvulana huyo, hivyo alitoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa
wananfunzi wengine wa kike.
Utetezi huo ulitupiliwa mbali na Mkuu wa Mkoa na kuagiza mwenyekiti
huyo akamatwe kwa kosa la kutoa adhabu ya upande mmoja huku akimwachia
huru mtuhumiwa wa kiume aliyemrubuni mwanafunzi huyo kufanya naye
mapenzi.
Habari zilizopatikana eneo la tukio zinadai kuwa baada ya walimu wa
shule ya Msingi Rungwa, kutilia shaka umiliki wa simu ya mkononi ya
mwanafunzi huyo, walimhoji na alikiri mwenyewe kupewa na mvulana huyo.
Walimu hao walidai kuweka mtego kwa mwanafunzi huyo kumpigia mvulana
huyo na kutokana na mazungumzo yao walibaini kuwa wana mahusiano ya
kimapenzi ya muda mrefu, hivyo kuamua kuwapeleka baraza la kata ambapo
mwanafunzi alitozwa faini na mpenzi wake kuachiwa huru.
Post a Comment