Mwacheni Kikwete apumzike
Rais wa Tanzania John Magufuli
amekanusha taarifa ambazo zimekuwa zikienea katika baadhi ya vyombo vya
habari na mitandao ya kijamii kwamba amezuia mziigo ya mke wa Rais
Mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete, Mama Salma.
Taarifa zimekuwa
zikidai taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), inayoongozwa na Mama
Salma, imeshindwa kulipia kodi mizigo mikubwa iliyoiingiza nchini
Tanzania na hivyo kuwa hatarini kupigwa mnada.
Aidha, habari hizo zilikuwa zimedai Rais Magufuli anahusika kuzuia mizigo hiyo bandarini mpaka hapo itakapolipiwa kodi.
Taarifa ya ikulu imesema Rais Magufuli hajawahi kuzuia wala kuagiza kuzuiwa kwa mizigo ya Mama Salma.
"Nimesikitishwa sana na uzushi unaofanywa dhidi ya Rais Mstaafu Dkt.
Jakaya Mrisho Kikwete na Mke wake Mama Salma Kikwete, tafadhali wale
mnaotengeneza uzushi huu acheni mara moja na muacheni Rais Mstaafu
Kikwete apumzike," amesema Dkt Magufuli, kwa mujibu wa taarifa kutoka
ikulu.
"Rais Mstaafu Kikwete amefanya kazi kubwa ya kulitumikia
Taifa hili, amestaafu anapumzika, narudia muacheni apumzike, Serikali
haitaendelea kuvumilia uzushi na uchonganishi huu unaofanywa kwa
makusudi ili kuwachafua viongozi wastaafu".
Dkt Magufuli amewataka
waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kuacha kuandika na
kuchapisha taarifa za uzushi na badala yake vizingatie weledi na kufuata
sheria.
Post a Comment