serikali ya kuanza kusambaza dawa katika hospitali zote nchini
AHADI ya serikali ya kuanza kusambaza dawa katika hospitali zote
nchini kutokana na madai ya kuwepo kwa uhaba wa dawa za aina mbalimbali,
imeanza kutekelezwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa ziarani mkoani Arusha amesema
Serikali imetoa Sh trilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa dawa na
kuhakikisha pia madaktari 8,000 wanasambazwa kwenye hospitali mbalimbali
za mikoa na wilaya ili kutatua changamoto za afya na utoaji wa huduma
bora kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amewataka watendaji wa Idara ya
Uhamiaji kufanya misako kwenye nyumba za wageni na kudhibiti wageni
wanaoingia kwenye mipaka mbalimbali nchini kutokana na kushamiri kwa
wahamiaji haramu.
Aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa
idara na taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo watumishi wa Halmashauri
ya Jiji la Arusha na Wilaya ya Arusha.
Ukosefu wa dawa.
Akizungumzia upatikanaji wa dawa, Majaliwa alisema serikali imetoa Sh
trilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa dawa za aina mbalimbali ili
kuondoa upungufu wa dawa kwenye hospitali nchini.
Akieleza namna serikali ilivyo na nia ya dhati ya kumaliza tatizo la
dawa nchini, Majaliwa alisema; “Awali tulitoa Sh bilioni 40 kwa ajili ya
dawa na sasa tumeongeza fedha hadi kufikia shilingi trilioni moja.
“Tunataka kero ya upungufu wa dawa hospitalini iishe. Naagiza kila
hospitali kuhakikisha inakuwa na dirisha la huduma za bure kwa wazee
pamoja na duka la dawa,” alisema.
Akizungumza kuhusu nidhamu ya fedha zinazotolewa na serikali kwa
ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika kila halmashauri alisema
serikali imeridhia kutoa Sh bilioni 177 kwa halmashauri zote nchini kwa
ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aliwataka wakuu wa idara, wakurugenzi, m
ameya pamoja na wakaguzi wa
ndani kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali zinakwenda katika
miradi ile iliyokusudiwa na si vinginevyo.
Alisema Mkoa wa Arusha umepokea Sh bilioni 54 katika halmashauri zote
kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kusisitiza kuwa serikali si kwamba
haina fedha ila imeminya matumizi ya hovyo hovyo yaliyokuwa yakifanyika
kwenye halmashauri au kubadilishwa fedha za matumizi ya miradi
iliyokusudiwa.
Alisisitiza kuwa ni vyema maofisa maduhuli kukusanya maduhuli ili
kuongeza mapato ya ndani yanayokusanywa ndani ya halmashauri ili
kuwezesha bajeti za halmashauri kutekeleza mambo mbalimbali.
Wahamiaji haramu
Kuhusu wahamiaji haramu, Waziri Mkuu alisema inashangaza kuona hivi
sasa kuna wimbi la watu wanaoingia katika maeneo mbalimbali ya mipakani
na kuleta madhara mbalimbali ikiwemo kuzagaa kwa silaha za aina
mbalimbali.
Alisema serikali haizuii wageni kutoka nje ya nchi kuingia nchini,
lakini ni lazima udhibiti wa wageni hao ufanyike kwa ukamilifu ili
kufahamu wanaingia nchini kufanya nini na wanakaa kwa siku ngapi ili
kudhibiti wingi wa watu wanaoingia nchini.
“Fanyeni misako kwenye nyumba za wageni na sehemu nyingine ili
kudhibiti watu wanaoingia nchini maana uingizwaji wa silaha zisizokuwepo
nchini umeongezeka. Ni lazima tujue zinaingia kwa nini,” alisema.
Uwajibikaji serikalini
Akizungumzia nidhamu katika utumishi wa umma, Waziri Mkuu aliwasihi
watumishi wa idara mbalimbali za serikali kuhakikisha wanafanya kazi kwa
nidhamu kwa kuwatumikia wananchi wanaohitaji huduma mbalimbali.
Alisema baadhi ya wananchi hawana uelewa juu ya wapi wapeleke
malalamiko yao, lakini kwa kuwa watumishi wa umma wapo, wanapaswa
kuwasikiliza na kuwapa maelekezo sahihi ni wapi waende ili matatizo yao
yatatuliwe na si kuwatolea maneno yasiyozingatia maadili.
“Serikali hii haitishi watumishi, hapana bali inasisitiza nidhamu ya
kazi makazini, hivyo ni lazima kila mtu afanye kazi kadri anavyotakiwa
kutekeleza majukumu yake. Serikali italipa madeni yote ya wafanyakazi
wanayoidai, kwani hivi sasa inamalizia kulipa madeni ya ndani halafu
watumishi watalipwa stahiki zao.”
Aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya kukagua miradi mbalimbali ya
maendeleo pamoja na kusoma vitabu vya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ili kuyafanyia kazi yale yote yaliyokuwepo katika idara
husika.
Alisisitiza Jiji la Arusha na halmashauri zote nchini kutenga maeneo
ya wazi ili kuwezesha wananchi kupata mahali pa kupumzikia, kwani hivi
sasa hakuna maeneo ya kupumzikia kutokana na kila mtu kujenga nyumba
hadi kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kwa ujenzi.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akisoma taarifa ya kwa
Waziri Mkuu, alisema mkoa huo unajitahidi kuhakikisha hali ya ulinzi na
usalama inaimarika.
Alisema hata hivyo unakabiliwa na upungufu wa walimu kwenye maeneo
yaliyopo pembezoni mwa miji na hivi sasa wanalifanyia kazi suala hilo
ili kuhakikisha walimu wanapelekwa kwenye shule zilizopo pembezoni.
Post a Comment