HATIMAYE imebainika kuwa chanzo cha ajali ya treni ya abiria ya Shirika la Reli Tanzania (TRL) iliyotokea katika eneo la Malagarasi mkoani Kigoma mchana jana, ni utelezi na kona kali katika eneo hilo.
Kutokana na ajali hiyo, majeruhi 21 wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, wakipatiwa matibabu. Treni hiyo ilikuwa ikitoka Tabora kwenda Kigoma.Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Martin Otieno alifafanua kuwa katika ajali hiyo hakukuwa na vifo huku akibainisha kuwa majeruhi wanaendelea vema.
Alisema katika ajali hiyo, injini ya treni na mabehewa mawili yalidondoka majira ya saa nane mchana ambapo wananchi walishiriki kuwaokoa abiria hao waliokuwa wamenasa katika mabehewa hayo. Kwa upande wake Kaimu Meneja Uhusiano wa TRL, Mohamed Mapondela alisema wataalamu wa shirika hilo wameshaenda kwenye eneo la tukio ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Alisema,”kwa sasa ninachoweza kusema ni kuwa hakuna taarifa za vifo ila kuna majeruhi tu na sababu ya ajali hiyo siweze kusema kwa kuwa wataalamu ndo wanalifanyia kazi kiundani suala hilo na taarifa kesho nitatoa”. Alisema kuwa kwa kawaida behewa moja linachukua abiria 80 na kwa hayo mawili yaliyotokea inamaanisha ni abiria 160 watakuwa wamehusishwa, lakini bado hawezi kusema moja kwa moja kama idadi hiyo ya watu walikuwemo ndani ya behewa wakati ajali inatokea.
Post a Comment