form two kuanza mtihani
form two kuanza mtihani
JUMLA ya watahiniwa 435,221 wamesajiliwa kufanya upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili huku watahiniwa 1,045,999 wakisajiliwa kwa ajili ya Darasa la Nne kwa mwaka huu.
Upimaji wa Kidato cha Pili umeanza jana hadi Novemba 25 katika shule za sekondari 4,669 wakati ule wa Darasa la Nne utafanyika Novemba 23 na 24 katika shule za msingi 17,032 Tanzania Bara.
Akizungumzia upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alisema idadi hiyo ni ongezeko la watahiniwa 38,451 ambayo ni asilimia 9.7 ya watahiniwa 396,770 waliosajiliwa mwaka 2015.
Dk Msonde alisema kati ya watahiniwa waliosajiliwa wavulana ni 214,013 sawa na asilimia 49.17 na wasichana ni 221,208 ambao ni asilimia 50.83 huku watahiniwa 67 ni wasioona na 306 wenye uoni hafifu.
Matokeo ya Kidato cha Pili mwaka 2015, yanaonesha kuwa wanafunzi 324,068 ambao ni sawa na asilimia 89 kati ya wanafunzi 363,666 waliofanya mtihani walifaulu na kuendelea na kidato cha tatu.
Kwa upande wa upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne, Dk Msonde alisema kati ya waliosajiliwa wavulana ni 507,732 sawa na asilimia 48.54 na wasichana ni 538,267 ambao ni asilimia 51.46 huku watahiniwa 76 ni wasioona na 483 kwenye uoni hafifu.
“Katika upimaji wa kitaifa wa mwaka huu kumekuwa na ongezeko la watahiniwa 8,694 ambao ni asilimia 0.8 ukilinganisha na watahiniwa 1,037,305 waliosajiliwa mwaka 2015,” alisema.
Matokeo ya Upimaji wa Darasa la Nne 2015 yanaonesha kuwa wanafunzi 869,057 kati ya wanafunzi 977,886 sawa na asilimia 88.87 waliofanya upimaji wamepata alama katika madaraja ya A,B,C na D huku wanafunzi 108,829 sawa na asilimia 11.13 wamepata alama za ufaulu usioridhisha.
“Maandalizi yote kwa ajili ya upimaji huo yamekamilika, ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mitihani na nyaraka zote muhimu katika mikoa na halmashauri zote za Tanzania Bara,” alisema na kuongeza kuwa upimaji wa Kidato cha Pili ni muhimu kwa wanafunzi ili kupima uwezo wa uelewa wa wanafunzi katika yale waliyojifunza kwa kipindi cha miaka mwili ya masomo na kwa Darasa la Nne ni kujua kiwango cha wanafunzi kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Aidha, Msonde amezitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na halmashauri au manispaa kuhakikisha kuwa taratibu za upimaji zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazingira ya vituo yapo salama, tulivu na kuzuia mianya ya udanganyifu na kwamba Baraza litachukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa upimaji wa Kitaifa.
Post a Comment