Header Ads

Dk John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni Kuu ya Ulinzi ya Jeshi la Ukombozi la Watu wa China




RAIS na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dk John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni Kuu ya Ulinzi ya Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA), Jenerali Fan Changlong, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, viongozi hao walikutana jana na wamezungumzia uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na China katika nyanja mbalimbali, ikiwemo katika masuala ya ulinzi ambapo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa na ushirikiano na Jeshi la Ukombozi la Watu wa China.

Ikulu imesema Rais Magufuli amemueleza Jeneral
i Fan kuwa Tanzania inathamini ushirikiano huo uliochangia kufanikisha juhudi za kuimarisha JWTZ zinazolenga kuwa na jeshi la kisasa na vifaa bora.
Dk Magufuli amemuomba Jenerali Fan Changlong afikishe salamu na shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na China katika kuimarisha majeshi ya ulinzi na pia katika masuala mengine ya maendeleo ya kijamii.
“Nimefurahishwa na ziara yako hapa nchini kwetu, ujio wako unazidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi zetu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa haya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Mwenyekiti Mao Tse-tung wa China. “Naomba unipelekee salamu zangu kwa Rais Xi Jinping na umwambie kuwa pamoja na kuendeleza uhusiano na ushirikiano wetu katika kuimarisha majeshi pia tunatarajia kuona China inakuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi zetu za maendeleo kwa kujenga viwanda na kushiriki katika miradi mingine ukiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani Standard Gauge,” alisema Rais Magufuli.

Naye Jenerali Fan Changlong amempongeza Rais Magufuli kwa uongozi imara aliouonesha katika Awamu ya Tano na amemhakikishia kuwa China itaendeleza na kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika masuala ya usalama hasa kuimarisha JWTZ.

Amesema PLA na JWTZ yana uhusiano wenye manufaa makubwa na kwamba hivi sasa yanafanya uboreshaji utakaoyaimarisha zaidi na kuwa majeshi ya kisasa.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange na makamanda wa majeshi wa Tanzania na China.

No comments