MTOTO mdogo mwenye umri wa miaka 3 kunajisiwa hadi kifo
MTOTO mdogo mwenye umri wa miaka mitatu mkazi wa Kijiji cha Nyamihaga Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma amekufa baada ya kunajisiwa na baba yake wa kambo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui alisema jana kwamba wamemtia mbaroni mtuhumiwa Hamimu Saidi (27) mkazi wa kijiji hicho cha Nyamihaga.
Akitoa maelekezo kuhusu mkasa huo, Kamanda Mtui alisema mtuhumiwa alitekeleza dhamira yake hiyo wakati mama wa mtoto huyo ambaye alikuwa mke wa mtuhumiwa alipokwenda kisimani kuchota maji.
Alisema baada ya mwanamke huyo kurejea nyumbani kutoka kisimani alimshuhudia mtoto wake akilalamika sana wakati akitaka kujisaidia haja ndogo na ndipo alipomchunguza akagundua kwamba mtoto huyo alikuwa ameingiliwa na kujeruhiwa kwenye sehemu zake za siri.
Kamanda Mtui alisema baada ya kugundua hilo, mama huyo wa mtoto alimchukua mtoto huyo na kumpeleka Hospitali ya Mkoa ya Maweni kwa matibabu, ambako iligunduliwa kuwa mtoto huyo alikuwa amenajisiwa na alikuwa amebanwa shingo wakati akifanyiwa kitendo hicho hivyo alikosa pumzi wakati akifanyiwa unyama huo.
Kamanda huyo alisema hata hivyo mtoto huyo alifariki katika Hospitali ya Mkoa ya Maweni alipokuwa akitibiwa na kwamba baada ya uchunguzi wa kidaktari na uchunguzi wa Polisi, mwili wa mtoto huyo ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.
“Kwa sasa mtuhumiwa Hamimu Saidi anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Kigoma wakati upelelezi ukiendelea ili taratibu za kumfikisha mahakamani zifanyike na kwamba anatarajia kufikishwa mahakamani wakati wowote upelelezi huo utakapokamilika,” alieleza Kamanda Mtui.
Post a Comment