WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako uhakiki wa vyeti vya vifo
WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa baada ya uhakiki wa vyeti vya vifo vilivyowasilishwa na wanafunzi wanaoomba mikopo wakidai kwamba ni yatima, watakaobainika kupeleka vyeti vilivyoghushiwa watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Hatua hiyo imekuja baada ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) hivi karibuni kubaini uwepo wa baadhi ya wanafunzi ambao wamewasilisha vyeti feki vya vifo vya wazazi wao ili waonekane kama ni watoto yatima, huku wakihitaji kupewa kipaumbele cha kupatiwa mkopo.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa elimu jana Dar es Salaam, Profesa Ndalichako alisema kwa wanafunzi ambao wanatambua kwamba walipeleka vyeti feki vya vifo na ripoti za daktari kuonesha kwamba wana magonjwa mbalimbali ambayo wanastahili kupewa mkopo, wajisalimishe kuepuka usumbufu watakaoupata.
“Timu yetu inaendelea na uhakiki na ripoti itakapokamilika kwa wale wanafunzi watakaobainika wameghushi vyeti vya vifo hilo ni kosa la jinai hivyo watashitakiwa,” alisema Profesa Ndalichako.
Alisema wapo watu wanaosema hii ni serikali ya uhakiki, na kueleza kwamba Watanzania wamezoea kudanganya hivyo wanachokifanya ni kujiridhisha ili mtu apate haki inayostahili na si vinginevyo. Alisema kama mtu ni yatima basi awe yatima kweli kweli, lakini wameona dalili kwa watu wanaoghushi ripoti za daktari na vyeti vya vifo ili waombe mikopo.
Aidha, alisema timu ya kukagua vyuo vyote nchini ikikamilisha ripoti yake vyuo ambavyo havitastahili kutoa kozi fulani au kutoa mafunzo yote, vitafungiwa. Alisema baada ya vyuo hivyo kufungwa serikali itachukua jukumu la kuwapeleka wanafunzi katika vyuo vingine ili kuendelea na masomo yao.
“Utaratibu wa sasa ni kwamba wanafunzi wanaomba kujiunga na masoko kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) hivyo endapo kutakuwa na vyuo vimefungiwa kutoa elimu jukumu la wanafunzi waliopo litachukuliwa na serikali kuona watawapeleka wapi wanafunzi waliopo,” alifafanua Profesa Ndalichako.
Hata hivyo, alitolea mfano Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph ambacho kilifungiwa Februari mwaka huu kwamba wanafunzi wote waliopelekwa kwenye vyuo mbalimbali walionekana hawana uwezo hivyo walitakiwa kurudia mwaka.
Kwa mujibu wa waziri huyo, baadhi ya wanafunzi waliopelekwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wamegoma kurudia mwaka na kueleza kuwa kama wanaendelea kugoma wakati uwezo wao ni mdogo, watafute kitu kingine cha kufanya.
Alisema wanafunzi wanapopelekwa kwenye vyuo mbalimbali watafanyiwa tathmini kama ataendana na wanafunzi waliopo na kama wataonekana hawana uwezo, watatakiwa kurudia mwaka na mtu asiyetaka atajiamulia cha kufanya.
“Hatuwezi kuendelea kama vyuo vyetu havina ubora na wakati tunataka kufikia uchumi wa kati kwa kuwa na viwanda. Katika mkutano huu wadau watazungumzia changamoto zilizopo sokoni kuona namna gani ya kuwawezesha kuwa na ujuzi na maarifa yenye tija ili kuendana na mazingira,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Eleuther Mwageni alisema matokeo ya ripoti yatakayotolewa ndiyo yataamua ni vyuo vingapi vinatakiwa kufungwa na programu zipi zifungiwe. Profesa Mwageni alisema hata kabla vyuo havijafungiwa wanafunzi wanaweza kuomba kuhamishiwa chuo kingine kwa kuwa suala hilo liko wazi.
“Tumeshirikiana na wadau mbalimbali kuandaa mkutano huu, tutazungumzia namna gani tutaboresha elimu ya juu, mbinu za kufundishia, vyuo kujitegemea na namna gani wanafunzi watapata ujuzi na ufundi katika kuchangia masuala mazima ya kufikia maendeleo ya viwanda,’’ alieleza.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Vyuo Vikuu nchini, Dk Thadeus Mkamwa alisema tamko la waziri lilianza kama fununu, lakini baadaye waliona uhakiki vyuo ukipewa kipaumbele.
Dk Mkamwa ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Augustine (SAUT), alisema kinachohakikiwa ni kwamba vipo baadhi ya vyuo ambavyo vilipewa ruksa ya kujiendesha kabla ya kukamilisha taratibu na vingine havijakidhi vigezo.
“Jambo muhimu ambalo kamati itatafakari ni namna vyuo vikuu vitakuwa na malengo mazuri ya baadae na mipango bora kwa kuwa na walimu wengi na vifaa vya kuendeshea vyuo hivyo. Watu wasione vyuo vinafungiwa bali vinaimarishwa na kuimarika kutokana na matamko hayo,” alisema Dk Mkamwa.
Post a Comment