Header Ads

MTU mmoja amekufa na wengine wawili kujeruhiwa baada ya kufunikwa na kifusi katika mgodi


Image result for PICHA YA JENEZA



MTU mmoja amekufa na wengine wawili kujeruhiwa baada ya kufunikwa na kifusi katika mgodi wa dhahabu wa Nholi uliopo wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Ernest Kimola tukio hilo lilitokea jana saa 9:00 alasiri kwenye mgodi huo.
Watu hao walikumbwa na mkasa huo kwenye moja ya mashimo yaliyopo kwenye mgodi huo.
Aliyekufa ni Doto Shoti. Akielezea tukio hilo alisema juzi saa 11:00 jioni katika kijiji cha Nholi katika mgodi wa dhahabu wachimbaji wadogo, watatu waliangukiwa na kifusi wakiwa wanachimba dhahabu.
Watu wawili waliokolewa wakiwa hai ambao ni Joseph Emanuel, mkazi wa Bahi na Elisha Donald ambaye ni mkazi wa Tabora huku mmoja akipoteza maisha.
“Imebainika kuwa chanzo ni kufunikwa na udongo na kukosa hewa kutokana na ardhi wanayochimba kukosa miamba imara na wananchi wawe waangalifu kwa kutanguliza usalama wao,” alisema Kaimu kamanda huyo na kuongeza kuwa juhudi za uokoaji zilichukua saa nne tangu wafunikwe na kifusi saa 11:00 jioni hadi kuokolewa saa 2:00 usiku.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa wilaya ya Bahi, Elizabeth Kitundu, alisema hali hiyo imetokana na mmomonyoko wa udongo na kuongeza kuwa ipo haja ya kuweka mpango madhubuti wa kuhakikisha halijitokezi tena tukio hilo kwa kufuata ushauri na maagizo ya wataalamu ili wanapochimba wawe na tahadhari.
Mmoja wa manusura Elisha Donald, alisema mkasa huo uliwakumba majira ya saa 9:00 alasiri ambapo walikuwa watatu ndani ya shimo hilo wakiendelea na uchimbaji, lakini baada ya muda waliona udongo ukidondoka kidogo kidogo.
“Tukashauriana tusimame pembeni ndipo ikaanguka ngema kubwa ya udongo na kutufunika,” alisema Donald na kuongeza kuwa baada ya muda wakiwa ndani ya shimo walikosa hewa lakini juhudi za ukoaji zilisaidia kuwatoa majira ya saa 1:00 usiku akiwa yeye na mwenzake mmoja hai, lakini mwenzao wa tatu tayari alikuwa amepoteza maisha.
Aidha alisema chanzo cha kifusi hicho kuanguka ni shimo la jirani lililokuwa na mawe yaliyolegea, hivyo kutokana na shughuli zilizoendelea lilitikisika na kusababisha maafa hayo. Kaimu Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma, Dk Ibenzi Ernest alithibitisha kupokewa kwa majeruhi hao wawili na mwili wa mtu mmoja aliyekufa.

No comments