Header Ads

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan kutokomeza ugonjwa wa tezi dume


Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi waliojitokeza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya uchunguzi wa saratani ya matiti pamoja na ya mlango wa uzazi kwenye Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza jana. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameiomba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuanzisha kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa tezi dume kutokana na idadi kubwa ya watu wanaofariki hivi sasa.
Aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti kwenye viwanja vya Furahisha jijini hapa.
Hakuingia kwa undani kuzungumzia ugonjwa wa tezi dume, lakini alibainisha kuwa kati ya watu saba, wanne wanafariki kutokana na tezi dume ambayo huwapata wanaume.
Katika siku za karibuni, ugonjwa wa tezi dume umetajwa kuwasumbua watu wengi nchini na duniani kwa ujumla, na wiki iliyopita, aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta alifariki duniani kwa ugonjwa huo. Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alikiri mwaka jana kupatwa na ugonjwa huo, lakini akatibiwa na kupona mapema.
Akizungumzia saratani ya kizazi na ya matiti, Makamu wa Rais aliishauri jamii hasa kinamama kupima afya zao ili kuepuka matatizo hayo, akisema saratani ya mlango wa kizazi imekuwa ikiongoza kwa vifo vya watu wengi sana ikifuatiwa na saratani ya matiti.
Aidha, alisema serikali imetenga Sh bilioni tano ili kujenga vituo vitatu vya afya katika kila halmashauri nchini ili kutokomeza tatizo la saratani ya shingo ya kizazi na ya matiti.
“Serikali pia imetenga shilingi bilioni saba za kununulia dawa za saratani ya matiti na shingo ya uzazi. Dawa za saratani ni ghali sana sisi kama serikali tunafanya kila jitihada kupunguza ughali wa dawa hizi za saratani. Kampeni hii ya upimaji wa saratani imeanza hapa Mwanza, Mewata (Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania) ijitahidi kampeni hii ifike mikoa mingine pia,” alisema.
Rais wa Mewata, Sarafina Mkuwa alisema chama hicho na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itaendelea kupambana kuboresha afya ya mama na mtoto, kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusu saratani hizo hatari ambazo zimekuwa zikiongoza kwa vifo vingi.
Kwa utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO), nchini kinamama na wasichana 7,000 wanaathirika na saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya matiti. Mkoa wa Mwanza una wagonjwa wa saratani ya matiti 3,000 na saratani ya shingo ya kizazi 12,000.

No comments