majoho kupewa eshema yake
WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imesema kuwa imeanza mchakato wa kuandaa waraka rasmi wa kuzuia majoho kutumika kwenye mahafali ya wanafunzi wanaomaliza Stashahada, huku ikisisitiza utekelezaji wa agizo hilo mara moja.
Waraka huo unatokana na agizo lililotolewa wiki iliyopita na Waziri, Profesa Joyce Ndalichako alipokuwa akiwatunuku vyeti wahitimu wa mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu kwa njia ya masafa iliyotolewa na Wakala wa Usimamizi na Uongozi wa Elimu nchini (ADEM) mkoani Mbeya.
Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Kamishna wa Elimu katika wizara hiyo, Venance Manori akizungumza na gazeti hili jana kuhusu agizo hilo lililotolewa na Profesa Ndalichako, alisisitiza wizara inaendelea na mchakato wa kuandaa waraka rasmi, lakini agizo hilo lililotolewa na waziri ni halali linapaswa kutekelezwa.
“Wahitimu wasio na sifa ya kuanzia Shahada ya Kwanza wanatakiwa wasivae majoho, waraka rasmi unaosisitiza agizo la waziri Ndalichako umeshaanza kuandaliwa,” alieleza Mkurugenzi Msaidizi Manori na kushauri taasisi zote zinazotoa elimu zianze kutekeleza agizo hilo mara moja.
Baada ya agizo hilo la Waziri Ndalichako, mapema wiki hii Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) ulitoa taarifa kwa wahitimu wake wa Stashahada ya Uongozi na Uendeshaji wa Elimu (DEMA) pamoja na Stashahada ya Ukaguzi wa Shule (DSI) katika chuo cha Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kuwa hakutakuwepo na uvaaji wa majoho kutokana na agizo hilo badala yake wahitimu hao wavae nguo nadhifu pamoja na skafu ya bendera ya taifa.
Lakini baada ya taarifa hiyo juzi ilitolewa taarifa nyingine mpya kuwa wanafunzi hao wanaruhusiwa kuvaa majoho kutokana na kauli ya waziri aliyoitoa kwamba agizo hilo litaanza baada ya kutolewa waraka rasmi.
Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa ADEM, Lameck Kagali alifafanua kuwa wamewaruhusu wanafunzi hao kuvaa majoho baada ya Profesa Ndalichako, kutamka kuwa utekelezaji huo utafanyika baada ya waraka kutoka rasmi.
Katika miaka ya karibuni, kumeibuka utaratibu wa vyuo pamoja na shule mbalimbali kuwavisha wahitimu wao, wakiwamo wanafunzi wa shule za awali, msingi na wanafunzi wa ngazi ya Cheti na Stashahada majoho ambayo kimsingi yalikuwa yakivaliwa katika vyuo vikuu na wanafunzi wanaohitimu kuanzia Shahada ya Kwanza.
Post a Comment