WATU wasiojulikana wamevuka uzio wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan Karume
WATU wasiojulikana wamevuka uzio wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan Karume na kufanya vitendo vya uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwamo kuchota mchanga kwa ajili ya ujenzi.
Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amaan Karume, Mussa Kitwana alisema uharibifu unaofanywa ni kuchota mchanga pamoja na kuchimba mawe kwa ajili ya kazi za ujenzi wa nyumba.
Alisema ni kosa kwa mujibu wa sheria za kiusalama za viwanja vya ndege kwa mtu yeyote kuingia ndani ya eneo hilo na kufanya shughuli za uharibifu wa mazingira ikiwemo kuchota mchanga.
Kitwana alisema matukio hayo yanarudisha nyuma juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kuimarisha huduma za uwanja wa ndege pamoja na kulinda maeneo yake kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwamo upanuzi wa uwanja.
Mmoja ya viongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege vya Zanzibar, Zaina Ibrahim alisema matukio ya watu kuvamia na kuingia katika eneo la uzio wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume yamekuwa yakijirudia mara kwa mara kwa nyakati tofauti.
Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege vya Zanzibar, Makame Abdalla aliwataka wananchi wanaoishi jirani na eneo la uwanja huo, kuheshimu na kuzingatia sheria za uhifadhi wa eneo hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Alisema kazi kubwa inayofanywa kwa sasa ni kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi jirani na uwanja huo kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira na kuepukana na vitendo vya kuchota mchanga ambavyo ni kosa.
Post a Comment