kuisababishia hasara serikali ya dola za Marekani 66,890, jana imeahirishwa.
HUKUMU ya aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Bernad Murunya na wenzake watatu ya kuisababishia hasara serikali ya dola za Marekani 66,890, jana imeahirishwa.
Akizungumza mbele ya Wakili wa TAKUKURU, Hamidu Sembano, Hakimu Patricia Kisinda wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha alisema ameshindwa kuisoma hukumu hiyo jana, kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake.
“Nawaomba samahani mpaka Desemba 6 mwaka huu nitaisoma, kuna vitu namalizia, ili siku hiyo niweze kutoa hukumu,” alisema.
Katika kesi hiyo, Hakimu Kisinda alimalizia kusikiliza ushahidi uliotolewa na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa wakati huo NCAA, Shad Kiambile ambaye ni mshitakiwa wa tatu na Mkurugenzi wa Kampuni ya usafirishaji wa anga ya Cosmos, Salha Issa, ambaye ni mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo.
Katika ushahidi wake Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Kiambile alieleza mahakama hiyo kuwa, hakuna hasara waliyosababishia serikali, kwa sababu fedha hizo zilifidiwa kwa safari za watu wengine, japo yeye hakuwepo kazini alikuwa amestaafu Januari mwaka 2013 wakati wa fidia hiyo.
Alisema anachokumbuka akiwa kazini bosi wake Murunya alimpa maelekezo ya kuandaa malipo ya safari ya aliyekuwa Waziri wa Utalii, Ezekiel Maige, Msaidizi wake Elgius Muyungi na Murunya mwenyewe na yeye alielekeza kwa Meneja wa Idara ya Utalii.
Mkurugenzi wa Kampuni ya utoaji huduma ya usafirishaji wa anga Cosmos, Salha Issa, aliiambia mahakama hiyo imuachie huru, kwa sababu kampuni yake haikula fedha hizo ila walifidia kwa watu watano na kwa kutumia ndege ya Emirates na KLM.
Aliwataja watu hao kuwa ni aliyekuwa Spika wa Bunge Job Ndugai ambaye alisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Canada Oktoba 18 mwaka 2011 (dola za Marekani 17,122), Bernad Murunya aliyesafiri kwenda Korea Oktoba 6, mwaka 2011 (dola 15,304), Peter Makutiani alikwenda Canada Oktoba 18/2011 (dola 14,260), Yusuph Machumu alikwenda Canada Oktoba 18/2011 (dola 14,260) na Donaltias Kamamba alikwenda Roma, Italia Novemba 7/2011 (dola 5,460).
Alisema cha kushangaza aliona barua kutoka kwa Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Fredy Manongi, 27 Januari mwaka 2014 wakiwakumbusha kurudisha fedha dola za Marekani 66,890, ambapo wao walijibu kwa barua ya Machi 14, mwaka 2014 kuwa hawadaiwi na walishalipa, huku akiambatanisha majina ya watu watano waliofidia safari zao.
Meneja wa huduma za utalii katika Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro (NCAA), Veronica Funguo (42) ambaye ni mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo amemaliza kutoa ushahidi wake.
chanzo habari leo
Post a Comment