Header Ads

Lema kusota rumande yupo inje ya Mahakama Kuu

Lema kusota rumande yupo inje ya  Mahakama Kuu



WANASHERIA wa serikali jana wamepinga tena dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema iliyokuwa wazi mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Desdery Kamugisha ambaye awali alitupa hoja za mawakili hao na kutaka kutoa masharti ya dhamana.

Wanasheria hao ambao ni Maternus Marandu na Paulo Kadushi walisema wamewasilisha pingamizi hiyo mahakamani hapo kupinga Lema kupewa dhamana hadi hapo mahakama kuu itakaposikiliza kesi ya msingi ndipo apewe dhamana.

“Mheshimiwa sisi tumewasilisha hoja hapa kuwa tunapinga Lema kupewa dhamana kwa sababu tumefungua kesi mahakama kuu kupinga Lema kupewa dhamana sasa tutashangaa mahakama hii ikimpa dhamana wakati kuna kesi imefunguliwa mahakama kuu,” alisema.

Kadushi pia alitoa nakala kwa Hakimu Kamugisha za kesi zilizotumiwa na mahakama mbalimbali ambazo zilikuwa zikitolewa uamuzi na kupingwa dhamana yake kwa sababu imefunguliwa kesi nyingine mahakama kuu.

Baada ya hoja hizo za Wakili Kadushi kuliibuka malumbano ya kisheria kwa mawakili wa Lema wakiongozwa na wakili Shadrack Mfinanga ambaye aliitaka mahakama hiyo kumpa dhamana Lema huku kesi hiyo iliyofunguliwa mahakama kuu ikipangwa kusikilizwa.

Mfinanga alihoji pia kwa nini wanasheria hao wazuie haki ya msingi ya Lema kupewa dhamana huku wakifahamu pingamizi zao dhidi ya Lema kupewa dhamana zimetupiliwa mbali na mahakama hiyo.

Kutokana na malumbano hayo ya kisheria hakimu aliahirisha kesi kwa dakika kumi kisha alirudi tena mahakamani hapo na kutoa uamuzi kuwa anaungana na hoja za mawakili wa serikali, kwani mahakama hiyo haiwezi kuamua kumpa dhamana Lema kutokana na Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) kufungua kesi ya kupinga maamuzi ya mahakama hiyo kumpa dhamana Lema.

Alisema kutokana na hoja hiyo anabanwa kisheria kwa sababu ni kweli mawakili hao wamewasilisha hoja hiyo mahakama kuu na yeye hawezi kuipinga, hivyo Lema ataendelea kuwa mahabusu hadi hapo Mahakama Kuu itakapotoa maamuzi kuhusu kesi hiyo iliyofunguliwa na kisha yeye atatoa dhamana iliyokuwa wazi hapo awali.

Awali kabla ya pingamizi Kamugisha alitoa uamuzi wa kumpa Lema dhamana yake jana mahakamani hapo na kusisitiza kuwa haoni sababu ya kutompa dhamana kwa sababu ametafsiri vifungu mbalimbali vya sheria na kubaini kuwa hakuna sheria inayomnyima dhamana mshitakiwa hata kama ana kesi mbili zaidi mahakamani.
Alisema pia hakuna kifungu cha sheria kinachomnyima haki mshtakiwa ingawa baadhi ya masharti ya dhamana kama yanakiukwa ndio mshtakiwa anaweza kunyimwa dhamana yake lakini amepitia hoja zote za mawakili wa serikali na mshtakiwa na amebaini hakuna kifungu cha sheria kinachozuia mshtakiwa kupewa dhamana.

Akiendelea kupangua hoja za mawakili hao wa serikali, Hakimu Kamugisha alitafsiri vifungu mbalimbali vya sheria na kubaini kuwa hakuna kifungu chochote cha sheria kinachomnyima haki mshtakiwa ya kuwa huru huku akisema hoja za mawakili hao wa serikali za kupinga Lema kupewa dhamana kwa sababu awali alikuwa na kesi nyingine mbili mahakamani hapo na alipewa dhamana lakini akiwa nje kwa dhamana mbunge huyo alifanya tena makosa kwa nyakati tofauti hazina mashiko.

Lema anakabiliwa na mashtaka mawili tofauti katika kesi namba 440/2016 anayodaiwa kuyafanya Oktoba 22/2016 maeneo ya Kambi ya Fisi Kata ya Ngarenaro katika mkutano wa hadhara.

Inadaiwa kuwa katika mkutano huo alitamka maneno yasemayo: “Rais Magufuli akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani ipo siku Taifa hili litaingia kwenye umwagaji wa damu, Rais yoyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria mpaka ya katiba, Rais huyo ataingiza Taifa katika majanga na umwagaji wa damu, watu watajaa vifua wakaamua kulipuka, jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu utakaojitokeza.”

Kesi ya pili inadaiwa kuwa maeneo ya Shule ya sekondari Baraa katika mkutano wa hadhara alitamka kuwa, “Kiburi cha Rais kikiendelea na Rais akijiona yeye ni mungu 2020 hatafika.” Wafuasi wa Lema walikuwa wakilia wakati anapanda gari kwenda mahabusu Kisongo.

No comments