Madereva watakiwa kulipa faini
Madereva watakiwa kulipa faini
MADEREVA wa vyombo vya moto wanaodaiwa na Kikosi cha Usalama Barabarani kutokana na faini mbalimbali wametakiwa kulipa faini hizo kabla ya Desemba 31, mwaka huu kwa kuwa wakishindwa kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Imebainika kuwa, Polisi kupitia kikosi hicho, inadai zaidi ya Sh bilioni tatu ambazo zinatokana na faini za makosa mbalimbali yaliyofanywa na madereva hao, ambayo huwa wanatakiwa kulipa ndani ya siku saba.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva wakati akifunga kilele cha maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani ya Kanda Maalumu ya Dar es Salaam yaliyofanyika jana katika viwanja vya Mwembe Yanga.
Lyaniva alisema madereva hao hawana budi kulipa fedha hizo kabla ya tarehe hiyo kwani baada ya hapo, watafuatiliwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Aliwataka askari wa usalama barabarani kupambana na madereva wakorofi na kuendelea kutoa elimu kwa watu wote, huku akionya abiria wanaoshabikia mwendo kasi.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Mrakibu Msaidizi, Solomon Mwangamilo alisema, pamoja na kiwango cha ajali kuonekana kupungua, bado wanafanya jitihada kuhakikisha zinapungua au kumalizika kabisa.
Post a Comment