SHERIA Ndogo zaidi ya 15 na Kanuni kadhaa zikiwemo za kuasili watoto zimekutwa na dosari
SHERIA Ndogo zaidi ya 15 na Kanuni kadhaa zikiwemo za kuasili watoto zimekutwa na dosari
SHERIA Ndogo zaidi ya 15 na Kanuni kadhaa zikiwemo za kuasili watoto zimekutwa na dosari kadhaa na huenda zikafutwa ikiwa serikali haitazifanyia marekebisho kama ilivyopendekeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.
Taarifa ya Kwanza ya Kamati hiyo ya Sheria Ndogo iliyotolewa bungeni na kuridhiwa bila kujadiliwa na wabunge mwishoni mwa wiki, ilieleza kuwa baadhi ya sheria zinakinzana na Katiba, sheria za nchi na zinakwenda kinyume cha haki za binadamu.
Baadhi ya sheria hizo ndogo ni pamoja na ya Uasili wa Watoto za mwaka 2012; Ajira za Watoto za Mwaka 2012; Mwenendo wa Mahakama za Watoto za mwaka 2014; Kuzuia na Kudhibiti Dawa za Kulevya za mwaka 2016; Uagizaji wa Pamoja wa Bidhaa za Petroli za mwaka 2015 na Hakimiliki.
Nyingine ni Biashara ya Bidhaa za Petroli katika Miji na Vijiji Tanzania Bara; Kilimo Kwanza na Usalama wa Chakula za Halmashauri ya Wilaya ya Geita za mwaka 2015/16; Uanzishaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii za Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe 2014/15; Kuhifadhi Barabara za Halmashauri ya Wilaya ya Babati; na ya Ustawi na Nidhamu kwa Wanafunzi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto mwaka 2015.
Imo pia ya Afya na Usafi wa Mazingira za Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro; Ushuru wa Madini ya Ujenzi na Chumvi za Halmashauri ya Wilaya ya Babati za mwaka 2015; Ushuru wa Mazao ya Misitu za Halmashauri za Wilaya ya Sikonge ya mwaka 2015; Afya na Usafi wa Mazingira za Halmashauri ya Wilaya ya Geita; na za Afya na Usafi wa Mazingira za Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.
Kuhusu Sheria Ndogo ya Uasili wa Watoto, Kamati ilieleza kuwa, kuna dosari zinazopaswa kufanyiwa marekebisho na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kufanya marekebisho kwa kuwa zina maneno ya kunyanyapaa. Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati hiyo, yapo maneno yameandikwa "mtoto ana kilema" ambayo kwa tafsiri yanaonekana yananyanyapaa. Kamati imeshauri yaandikwe "mtoto mwenye ulemavu.”
“Kwa madhumuni ya kulinda ustawi wa watoto wanaoasiliwa nje ya nchi, Kamati inashauri Kanuni ziweke bayana utaratibu ambao taarifa za mtoto zitafuatiliwa kwa kuhusisha pia Balozi zetu," ilishauri Kamati hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), akiwasilisha taarifa hiyo ya kwanza ya Kamati hiyo, alisema mapendekezo ya kamati kuhusu uasili na masuala ya mtoto yanalenga kuhakikisha kila kanuni inayotungwa chini ya sheria ya mtoto, maslahi ya mtoto yanakuwa ndio msingi wa kuzingatiwa.
Katika Sheria Ndogo za Ajira za Watoto chini ya Sheria Mama ya Mtoto ya mwaka 2009, sheria hiyo mama imeweka masharti kuhusu haki ya mtoto kufanyakazi, makatazo na mazingira ambayo mtoto hapaswi kufanyakazi, haki za mtoto anayefanya kazi na utaratibu wa ufuatiliaji ustawi wa mtoto anayefanyakazi.
Aidha, katika uchambuzi wake, Kamati ilibaini kuwa, Sheria Ndogo hiyo haijataja kifungu cha Sheria Mama kinachotoa madaraka ya kutungwa kwa Sheria hiyo Ndogo na kuagiza serikali kufanya marekebisho.
Kuhusu Sheria ya Mwenendo wa Mahakama za Watoto, Ngeleja alisema Kamati ilibaini hakukuwa na sharti la kuwepo mtu wa kumsindikiza mtoto anapoitikia mwito wa Mahakama na kutaka sharti hilo liwepo.
Akizungumzia Sheria Ndogo ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Ngeleja alisema Kamati imeshauri kufanyike marekebisho kuzuia mazingira ambayo mali iliyotaifishwa kutokana na biashara ya dawa za kulevya inaweza kurudishwa kwa mmiliki.
Kamati pia ilishauri Wizara ya Nishati na Madini kuifuta Sheria Ndogo ya Biashara ya Bidhaa za Petroli Mijini na Vijijini Tanzania Bara kwa kuwa Kanuni ya 11 (3) inaweka adhabu ya faini ya Sh milioni tano kwa kosa la kuendesha shughuli bila kibali kwani iko kinyume cha adhabu katika Sheria Mama ya Petroli iliyoweka adhabu ya faini ya fedha isiyopungua Sh milioni 20.
Ngeleja alisema Sheria Ndogo ya Kilimo Kwanza na Usalama wa Chakula za Halmashauri ya Wilaya ya Geita za mwaka 2015/16 inakiuka haki za binadamu na Katiba kwani zinamlazimisha mfugaji kujiunga na vyama vya wafugaji na wajasiriamali jambo lililo kinyume na Ibara ya 20 (1) ya Katiba inayompa kila mtu haki na uhuru wa kushirikiana na watu wengine kwa hiyari yake mwenyewe.
Alisema zipo sheria ndogo zinazokwenda kinyume na Sheria Mama zikiwemo za Ushuru na Mazao ya Misitu za Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge; Ushuru wa Madini ya Ujenzi na Chumvi za Halmashauri ya Wilaya ya Babati ambazo faini zake zinakinzana na Sheria Mama.
“Kamati inashauri Ofisi ya Rais, Tamisemi ifanye marekebisho katika Sheria Ndogo zote za halmashauri zilizo kinyume na Sheria Mama kwa kuvifuta na kuviandika upya vifungu vyenye adhabu kubwa kuliko viwango vya sheria mama," alisema Ngeleja akisoma taarifa ya Kamati, bungeni.
Alisema ikiwa taasisi husika za serikali hazitachukua hatua za kurekebisha dosari zilizojitokeza katika uchambuzi huo, Bunge linaweza kutoa azimio la kuzuia kutumika kwa Sheria Ndogo husika na hata kufutwa ikibainika haikidhi matakwa ya Katiba.
Kutokana na dosari zilizokutwa katika Sheria Ndogo hizo na kanuni nyingine, Serikali kupitia wizara, halmashauri na taasisi zake, zimetakiwa kufanyia marekebisho mapendekezo hayo ili kuondoa muingiliano wa Katiba, Sheria Mama na sheria nyingine za nchi vinginevyo zitafutwa.
Post a Comment