VYAMA KUFUTWA KWA KUKOSA SIFA
VYAMA KUFUTWA KWA KUKOSA SIFA
WIKI iliyopita Msajili wa Vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi alivifutia usajili wa kudumu vyama vya siasa vitatu kutokana na kupoteza sifa za usajili wa kudumu kwa kukiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa.
Vyama vilivyofutiwa usajili wa kudumu ni pamoja na Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA), chama cha The African Progressive Party of Tanzania (APPT-Maendeleo) na chama cha Jahazi Asilia.
Kwa mujibu wa kanuni za msajili, endapo chama kinashindwa kutimiza sifa ya kuendelea kuwepo kwake kwenye usajili, vinafutwa. Vyama hivyo vitatu vilifutiwa usajili baada ya kubainika kuwa na mapungufu ya kutokuwa na ofisi ya chama Tanzania Bara na Zanzibar, kutokuwa na wanachama Zanzibar, kushindwa kuweka kumbukumbu za mapato na matumizi ya chama.
Mapungufu mengine ni kushindwa kuwasilisha hesabu zao za mapato na matumizi ya mwaka kwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ili zikaguliwe, kushindwa kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa tamko la orodha ya mali za vyama vyao na kushindwa kutekeleza matakwa kwamba mapato yote ya fedha ya chama yawekwe katika akaunti ya chama.
Si kwamba vyama vingine ni visafi kwa kiwango kikubwa namna hiyo, yawezekana vina changamoto mbalimbali ambazo kwa namna moja hadi nyingine zimekuwa zikiwakwaza hata wanachama au wafuasi wao au hata Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Licha ya vyama hivyo vilivyofutiwa kutambua kuwa havitekelezi matakwa ya sheria, lakini vilikuwa vikifanya kazi na hata wakati mwingine kusimamisha wagombea kwa ajili ya kugombea nafasi mbalimbali zikiwemo za juu za ubunge na urais.
Hatua hiyo iwe fursa kwa vyama vilivyobakia kuendelea kutekeleza matakwa ya sheria ya vyama vya siasa kama ilivyo, ili kuepuka kufutwa. Ikumbukwe kuwa Msajili alivifuta vyama hivyo kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa namba 5,1992.
Kwa ujumla vyama vilivyobaki vinapaswa kuheshimu Katiba na kanuni za vyama vyao, ili kuepusha migogoro ndani ya vyama, ambayo inafanya viwe dhaifu.
Haina ubishi kuwa hadi sasa vipo baadhi ya vyama ambavyo migogoro na migongano vimekuwa wakiiona kama sehemu ya maisha ya vyama hivyo, wengine wakipelekana hadi Mahakamani na hata wengine wakiishia kubaki wakilalamika kuhusu uongozi wa chama fulani.
Vyama vya siasa vinatakiwa kutambua kuwa migogoro haijengi wala kuviimarisha, bali ni eneo mojawapo ambalo linaweza kusababisha kwa kupungua kwa wanachama.
Hakuna mwanachama anayependa kusikia kuwepo kwa migogoro ya ndani kwa ndani katika vyama au baina ya mtu na mtu, wengi wao hupenda kusikia chama kikiwa kinafuata na kuzingatia sheria na kanuni walizojiwekea wakiamini kuwa ndio njia pekee ya kujiimarisha katika kufikia lengo wanalotaka.
Ikumbukwe kuwa uanzishwaji wa vyama vingi vya siasa nchini mwaka 1992, haukuwa na lengo la kuanzisha chama halafu kifikie hatua ya kufutwa kutokana na kushindwa kutimiza taratibu mbalimbali za usajili.
Kila anayekuwa na maono ya kuanzisha chama anakuwa na malengo yake, na kwa mantiki hiyo pia kiongozi wa chama anatakiwa kufuata taratibu zinazotakiwa ili kwamba aendelee kuaminiwa na wanachama aliowashawishi kwa ajili ya kuwa wafuasi wa chama hicho pindi anapokuwa ameanzisha chama hicho.
Kwa upande wa vyama vilivyofutiwa hata kama viongozi wa vyama hivyo walijisahau kutekeleza kile walichotakiwa lakini kwa mujibu wa Msajili wa Vyama vya Siasa, anasema kila chama kilipewa taarifa ya nia ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufuta usajili wa kudumu na kutakiwa kueleza kwa nini kisifutwe.
Hata hivyo ilielezwa kuwa katika utetezi wao vyama hivyo vilishindwa kutoa sababu za kuridhisha kuwa havijakiuka sheria na bado vinavyo sifa za usajili wa kudumu.
Post a Comment