Header Ads

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka viongozi wa Afrika kujiuliza wanaweza kuchangia kitu gani kuboresha maisha

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka viongozi wa Afrika kujiuliza wanaweza kuchangia kitu gani kuboresha maisha ya mamilioni ya wakazi wa bara hilo.

Image result for picha ya waziri mkuu


Aliwapa swali hilo juzi usiku wakati akizungumza na wawakilishi wa taasisi za kimataifa waliohudhuria uzinduzi wa taarifa ya Taasisi ya Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji Barani Afrika (ICF) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu aliyekuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo, alisema taasisi hiyo imesaidia kukuza uwekezaji kupitia miradi katika nchi mbalimbali za Afrika kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi, usajili wa biashara za wajasiriamali na upatikanaji wa leseni za biashara.
“Kutokana na kazi inayofanywa na taasisi hii, hali ya uwekezaji katika nchi nyingi imeimarika na bara la Afrika limekuwa mbia kwa wawekezaji kutokana na ushirikiano baina ya Serikali za nchi husika na sekta binafsi. Uchumi wa nchi nyingi za Afrika umeimarika kuliko ilivyokuwa awali,” alisema.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema zaidi ya wajasiriamali 500 kutoka Tanzania walipewa mafunzo kwa ushirikiano kati ya ICF, Serikali na Taasisi ya vyuo vikuu vya Afrika Mashariki na Kusini (ESAURP) ili kuwajengea uwezo wafanye biashara zao kwa tija zaidi. Alisema mafunzo hayo yaliwalenga wajasiriamali wadogo na wa kati wanaojihusisha na uvuvi, biashara za rejereja na jumla kutoka mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam.
Zaidi, alisema kupitia mafunzo hayo wajasiriamali hao waliweza kusajili na kurasimisha biashara zao, kuongeza mitaji na kujua namna ya kutunza taarifa za biashara hizo.
Mapema, Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo ambaye pia ni Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alisema kuna haja ya wananchi kubadili mitazamo juu ya sekta binafsi kwa sababu ina umuhimu katika ujenzi wa uchumi kwa nchi yoyote.
“Watu wengi wanahisi kwamba wawekezaji ni wabaya. Hii si kweli. Tunapaswa kujenga mazingira ya kuwakubali kwa sababu wanakuja na mitaji yao na wao wanawakilisha michango kutoka kwa mamilioni ya wafanyakazi kutoka kwenye nchi zao. Hatupaswi kuwaona kwamba ni maadui,” alisema Mkapa.
Alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kukubali kuiruhusu taasisi hiyo ya ICF iweke Makao Makuu yake nchini wakati ilikuwa imeshakataliwa kufanya hivyo katika nchi nyingi ilikopeleka maombi.
Aliwataka viongozi mbalimbali watumie uzoefu uliowekezwa na taasisi hiyo kwenye uboreshaji wa mifumo ya mahakama na ukusanyaji kodi, utoaji wa leseni na urasimishaji wa biashara za wajasiriamali wadogo.

No comments