Header Ads

'Freemason' mbaroni akituhumiwa kubaka,



POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam wamemkamata mkazi wa Mwenge jijini humo, Rajabu Mohamedi (25) maarufu kwa jina la Rajeshi, kwa tuhuma za kufanya unyang’anyi wa kutumia nguvu, kubaka wanawake na kuwadhalilisha.
Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amewaeleza waandishi wa habari leo kuwa, mtuhumiwa huyo alikamatwa jana Februari 25 saa 4.30 usiku maeneo ya Kinondoni akiwa anatumia gari namba T 172 BLH aina ya Fun Cargo.
Kamanda Mambosasa amesema, mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwakamata wanawake kwa nguvu na kuwaingiza kwenye gari na kuwalaghai kuwa ni mfanyabiashara na wakishaingia hutumia nguvu kuwanyang’anya vitu vilivyomo ndani ya pochi zao.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya kufanya hivyo mtuhumiwa huwazungusha wanawake hao barabarani huku akiwatisha kuwa yeye ni ‘Freemason’ na kuwa atawaua kwa kuwanyonya damu au kuwakata sehemu za miili yao.
“Kupitia vitisho hivyo, huwalazimisha wanawake hao kutoa namba zao za siri ‘password’ ya simu zao pamoja na za kadi zao za benki na kwenda kuwaibia fedha zao kwenye ATM, baada ya hapo huwaingilia na kuwafanyia udhalilishaji na kwenda kuwashusha na kuwatelekeza kwenye vichochoro” amesema.
Amesema wanawake wengi wamefanyiwa hayo lakini ni wachache wenye ujasiri walitoa ripoti kuhusu matukio hayo na ndipo polisi walipofuatilia na kumkamata mtuhumiwa.
“Mtuhumiwa huyu amekuwa akisaidiana na wenzake ambao bado tunawatafuta na wamekuwa wakiwafanyia wanawake ukatili, mpaka sasa tu kesi tatu ambazo zimeripotiwa…tunakamilisha taratibu za ushahidi ili tuweze kumfikisha mahakamani” amesema Kamanda Mambosasa.

No comments