TATIZO la maji nchini limemfanya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Issack Kamwelwe kuwa katika wakati mgumu
TATIZO la maji nchini limemfanya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Issack Kamwelwe kuwa katika wakati mgumu baada ya wabunge wengi kutaka wapatiwe majibu kwa kuomba mwongozo baada ya Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM), kuibua hoja ya tatizo la maji katika jimbo lake lililosababishwa na kukatwa umeme.
Akitoa hoja hiyo, Bashe, aliwataja Mawaziri wa Wizara ya Fedha na Mipango, Maji na Umwagiliaji, Nishati na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kuwa wamekuwa chanzo cha mateso na mahangaiko kwa wananchi wa Nzega, hivyo akasema lolote litakalotokea walaumiwe wao.
Bashe aliwataja hadharani Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango, Waziri wa Nishati Dk Medadi Kalemani, Waziri wa Maji na Umwagiliaji Isack Kamwelwe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) Suleiman Jafo kwamba, wamesababisha wananchi wa jimbo lake kukosa maji kwa siku ya 13 mfululilo wakati halmashauri hiyo haidaiwi hata shilingi moja.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo, alipoomba Mwongozo akitumia Kanuni ya 47 kuhusu jambo la dharura bungeni na alipopewa nafasi, alisema amekuwa akiwasiliana na serikali, lakini hakuna kinachoendelea na wahusika wamekaa kimya.
“Ndugu zangu wabunge na hasa wabunge wa CCM, naombeni mniunge mkono katika jambo hili, Nzega ni siku ya 13 sasa hatuna maji, wanawake wanateseka bila maji na kunilazimu ninunue maji kwa ajili ya hospitali,” alisema Bashe huku akionesha hisia kali.
Alisema ni mateso kwa wananchi wake, lakini serikali haijawahi kupeleka majibu ya aina yoyote kuhusu mateso hayo na bado inaonekana kutojali licha ya bunge kutaka wakutane na mbunge kujadiliana.
Alisema, inasikitisha kuona kuwa serikali ndiyo iliyofanya makosa, kwa kutopeleka fedha za maji kwa zaidi ya miaka tisa na kufanya halmashauri hiyo ikatiwe umeme na kukosa maji.
Hoja ya Bashe iliungwa mkono na wabunge wengi wa upinzani, huku wale wa CCM wakiwa wachache na kuchangia miongozo sita, kati ya tisa, ikitaka majibu ya matatizo ya maji; huku wengine wakisisitiza suala hilo lijadiliwe ndani ya Bunge hilo.
Waziri wa Nishati, Dk Kalemani alikiri Nzega kudaiwa kiasi cha Sh milioni 320 na kuwa alishaagiza Mkurugenzi wa Nzega azungumze na watu wa Tanesco ili wawashiwe umeme, lakini amekataa.
“Nimekutana na Bashe mara nne, mara mbili kabla ya suala hili kuibuka jana (juzi) na mara mbili baada ya suala hilo kuibuka,” alisema. Akijibu hoja hiyo na wakati wa kujibu miongozo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alielezea kwa upana ukubwa wa tatizo la maji kuwa ni la nchi nzima, hivyo ni tatizo kubwa ambalo halitakiwi kupuuzwa, akaomba mawaziri kuwatendea haki wananchi katika maeneo yote.
Chenge pia alimuomba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Ajira Jenister Mhagama, kukutana na mawaziri wa Maji, Nishati na Fedha mara baada ya kuahirishwa kwa shughuli za bunge mchana jana ili kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Hata hivyo, kabla ya kuahirishwa kwa kikao hicho, Bashe alionekana katika meza ya Waziri Mhagama wakiwa na Kalemani, Jafo, Juma Aweso (Naibu Waziri wa Maji) na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji.
Bashe alipingana mara kadhaa na Mhagama, kiasi cha kumfanya Chenge kuingilia kati ili kupunguza mivutano ya wawili hao, ambayo kila mmoja alionekana kutomwelewa mwenzake.
Baada ya majibu hayo, wabunge wengi walisimama na kuomba miongozo huku Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), akieleza tatizo la maji kuwa ni kubwa hata katika wilaya yake, ambako watumishi walikula fedha za mradi wa maji, lakini wakahamishwa na kuacha mradi ukiwa haujakamilika.
Pia Mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete (CCM), alielezea masikitiko yake kuwa anapouliza masuala ya maji, anajibiwa kisiasa na Waziri Kamwelwe, jambo alilosema linampa kero kubwa, kwani anazijua sheria na mwongozo, kwa kuwa amesomea mambo ya sheria, lakini anapodanganywa inamuuza.
Mwenyekiti, Chenge alizima moto huo, akisema mambo yote yanatakiwa kuchukuliwa na serikali na kisha kufanyiwa kazi, kabla ya wahusika kupelekewa majibu kwa uhakika. Wengine waliozungumzia suala la maji ni Mbunge wa Kawe Halima Mdee (Chadema), Mbunge wa Ukonga Mwita Waitara (Chadema), Mbunge wa Tanga Mjini Mussa Mbaruk (CUF) na Mbunge wa Mbulu Vijijini, Fratei Massay (CCM).
Post a Comment