Header Ads




JESHI la Polisi wilayani Nkasi katika Mkoa wa Rukwa limefanikiwa kuvunja ndoa ya msichana mwenye umri wa miaka 15 aliyekuwa tayari amelipiwa mahari ya ng'ombe 45 ili aolewe.
Msichana huyo alikuwa amefaulu na kupangiwa kujiunga na Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Nkomolo wilayani Nkasi Januari, mwaka huu lakini wazazi wake waliamua kumuozesha kwa mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 45 na 50.
Akizungumza na gazeti hili Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Nkasi (OCD) David Mtasya alisema kuwa mwanafunzi huyo wa kike alikuwa amechaguliwa na kupangiwa kujiunga na Shule ya Sekondari Nkomolo iliyopo mjini Namanyere wilayani humo.
"Kufuatia msako wa kuwasaka wanafunzi walishindwa kujiunga na shule wakizopangiwa kuanza kidato cha kwanza, polisi walimkuta msichana huyo katika kijiji cha Kanazi akiwa katika maandalizi ya kufunga ndoa ambapo wazazi wake walikuwa tayari wamepokea ng'ombe 45 ikiwa ni mahari," alisema.
Alisema kuwa, busara ilitumika na kuwa wazazi wa msichana huyo hawakutiwa mbaroni na polisi, lengo likiwa ni kumwezesha binti akajiunge na masomo ya Kidato cha Kwanza.
Aliongeza kuwa hivi sasa msichana huyo ameanza masomo yake katika shule hiyo ya Sekondari ya Nkomolo huku Jeshi la Polisi likiendelea kumsaka mwanaume aliyetaka kumuoa ambaye alikimbia na kujificha kusikojulikana

No comments