Header Ads

siri ya fichuka



Related image


HATIMAYE mwarobaini wa uporaji wa viwanja kwa wananchi wanyonge katika Jiji la Dar es Salaam, umepatikana baada ya serikali kuamua kutoa viwanja 600 kwa wananchi, waliobainika kuporwa viwanja hivyo kimakosa.
Jana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema tayari wananchi 600 wamepatiwa viwanja mbadala wa vile walivyokuwa navyo awali, baada ya watu kuvamia maeneo hayo na kuyaendeleza.
Alisema pia kuwa Mkoa wa Dar es Salaam, unaongoza kwa migogoro ya viwanja maeneo ya mijini kuliko mikoa mingine nchini. Aidha, alisema wizara hiyo imejipanga kuhakikisha mwaka huu inamaliza kero zote za migogoro ya ardhi nchi nzima kupitia kampeni ya Funguka kwa Waziri. Akizungumza wakati akisikiliza kero za wananchi wa Mkoa huo jana, Lukuvi alisema kuwa wananchi wamekuwa wakivamia viwanja vilivyopimwa na visivyopimwa pamoja na umilikishaji wa kiwanja kwa mtu zaidi ya mmoja.
Alisema maeneo yanayoongoza kwa migogoro ya viwanja ni Tegeta na Mbezi wilayani Kinondoni na kwamba changamoto hiyo, imesababishwa na watumishi wa serikali. “Awali tulisikiliza watu wasiopungua 400 na awamu hii tunasikiliza watu zaidi ya 420 wote wa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya hapa tutakwenda Kagera, Pwani na Kahama, hii ni njia mojawapo ya kusikiliza kero za wananchi kuhusu ardhi,” alisema Lukuvi.
Alieleza kuwa tayari wananchi 600 wamepatiwa viwanja mbadala wa vile walivyokuwa navyo awali baada ya watu kuvamia maeneo hayo na kuyaendeleza. Alifafanua kuwa wananchi waliofutiwa maeneo yao wamepewa viwanja mbadala wa vile walivyokuwa wanamiliki na watu ambao wamefanya uendelezaji wa viwanja wanaachiwa eneo kwa kulipa fedha kulingana na bei ya soko.
“Kumekuwa na kero za muda mrefu na tayari tumeunda idara ya kushughulika na kero hizo nami nitazisikiliza hadi zitakapoisha kote nchini. “Wataalamu wa ardhi wa Halmashauri na Wilaya watafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na Mabaraza ya Kata na Mahakama yatafanya kazi yake ipasavyo,” alisisiza.
Moja ya kundi lililofika kutoa kero zao, likiwakilishwa na Mwenyekiti wao wa Chama cha Wasanii wa Uchongaji Tanzania, Isihaka Abdul ambaye alisema kuwa eneo la Mwenge Vinyago limekuwa na migogoro kwa muda mrefu baada ya kundi la wafanyabiashara kutaka umiliki wa eneo hilo.


Abdul alisema kwa zaidi ya miaka 30, walipata ofa kutoka serikalini ya kumiliki eneo hilo, ambayo wamekuwa wakiilipia na kwamba kukosekana kwa hati kumesababisha wafanyabiashara kumega eneo. “Sisi tupo zaidi ya 400 lakini tuliofika hapa ni 25 pekee na wenzetu kutoka kundi la Makonde Handcrafts Village wameshindwa kufika, tunaomba utusaidie,” alisema Abdul.

No comments