Header Ads

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliahirisha Bunge leo hadi April 3, 2018




Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliahirisha Bunge leo hadi April 3, 2018. Katika hotuba yake ya kuahirisha bunge, Majaliwa amegusia mambo mengi ya utendaji pamoja na matarajio ya serikali katika mwaka huu wa fedha.
Katika kuhakikisha serikali inatekeleza ahadi zake kwa wananchi, Majaliwa amewataka watendaji wa kada zote serikalini wasitumie vitisho na ubabe katika utendaji wao ili watoe huduma bora kwa wananchi na hatimaye kumaliza kabisa kero za wananchi.
Kwa upande wa nishati nchini, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imepanga kusambaza umeme wa gridi katika vijiji zaidi ya 7,000 pamoja na vijiji zaidi ya 7500 kusambaziwa umeme usio wa gridi katika mpango wa REA lll ambapo utawasaidia wananchi kwa kiasi kikubwa kwa kuwa umeme ni hitaji kubwa sana.
Kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kujengwa kwa ukuta katika mgodi wa Mererani, Majaliwa amesema ujenzi wa ukuta huo wenye urefu wa zaidi ya kilomita 20 upo katika hatua za mwisho wilayani Simanjiro mkoani Arusha.
Kwa upande wa miundombinu,Waziri Mkuu amesema barabara zaidi ya 50 nchini zimeathirika katika mikoa mbalimbali nchini kutokana na mvua zilizonyesha mwishoni mwa mwaka jana na Manzoni mwa mwaka huu ambapo baadhi ya barabara hazikupata hitilafu na zilitumika kama kawaida wakati wote wa mvua.
Kwa upande wa Elimu Waziri Mkuu Kasim Majaliwa amesema sSerikali imepeleka moja kwa moja bilioni 124 katika kugharamia elimu bure kwa shule za Msingi na sekondari nchini. Amewahimiza wazazi kuhakikisha wanaitumia fursa hii kwa kuhakikisha wanapeleka watoto shuleni wakapate elimu iliyokusudiwa na serikali.
Kuhusu michango mashuleni, Majaliwa amesema inaruhusiwa kwa mtu mmoja mmoja, kikundi cha watu au taasisi kwa ujumla. Amesema michango hiyo ipelekwe kwa wakurugenzi ili ashirikishe bodi za shule na walimu wasisumbuliwe badala yake waachwe wajikite katika ufundishaji.

No comments