Header Ads

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema hatatoka katika wizara



WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema hatatoka katika wizara hiyo kwa tuhuma za rushwa ya ugawaji vitalu, kama ilivyowahi kutokea kwa baadhi ya mawaziri, waliowahi kuiongoza wizara hiyo.
Amesema pia kuwa serikali inaanzisha utaratibu wa ugawaji wa vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada kuanzia mwaka huu.
Akizungumza hivi karibuni, Dk Kigwangalla alisema mnada huo utafanyika kwenye mtandao (online) huku kila mtu akiona unavyokwenda.
Alisema vitalu vya kwanza vitagawiwa Julai Mosi, mwaka huu na kila mmoja atashuhudia. Watu watashindana na mshindi atapata kitalu.
"Katika nchi zote zenye rasilimali ya wanyamapori zinazoruhusu uwindaji Kusini mwa Jangwa la Sahara, tulibaki sisi tu tunaotumia huu utaratibu wa undugunaizesheni. Wenzetu wanatumia mnada na bahati nasibu.
"Utaratibu huu tutauwekea miongozo, kanuni na tutaweka mfumo wa kompyuta... Nikasema hapana mimi sitakuwa Waziri wa namna hiyo kwa kutofuata misingi iliyowekwa kisheria au kwa kuchukua rushwa, nikasema lazima tuweke utaratibu ulio wazi utakaoondoa mashaka ya rushwa kwenye vitalu."
Alisema Kifungu cha 38 kidogo cha 11 cha Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009, kinampa mamlaka Waziri wa wizara hiyo kugawa vitalu vya uwindaji na inamtaka kugawa kwa utaratibu wa wazi na kufuata misingi ya utawala bora.
"Kilichokuwa kinasababisha ni hicho kifungu, mamlaka ipo kwa Waziri kwa hiyo kama nakufahamu ukiomba nakupa kitalu, urafiki na waziri ndicho kilikuwa kigezo cha kupata kitalu," alisema Dk Kigwangalla.

No comments