Header Ads

RAIS John Magufuli amemtaka Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam Jackson Sosthenes Jackson kuwa askofu wa wote




RAIS John Magufuli amemtaka Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam Jackson Sosthenes Jackson kuwa askofu wa wote, kuvunja makundi yaliyokuwepo katika dayosisi hiyo, kutolipiza kisasi na kusamehe yote yaliyopita na badala yake ajenge dayosisi imara na aongoze kwa haki na upendo kwa wote.
Magufuli alisema hayo na kunukuu maneno kutoka katika Kitabu cha Biblia cha Mathayo 18:21-34 ambayo yanayosema:”Kisha Petro akamwendea akamwambia, bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? hata mara saba?
Yesu akamwambia, sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini...,”. Magufuli aliagiza hayo jana alipokihudhuria Ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu wa Tano wa Dayosisi ya Dar es Salaam Askofu Jackson Sosthenes Jackson katika Kanisa Kuu la Mtakatifu, Albano Upanga.
Jackson, alisimikwa baada ya aliyekuwepo askofu wa kanisa hilo Dk Valentino Mokiwa kuacha nafasi hiyo kwa kuagiza kufanya hivyo na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Jacob Chimeledya.
Katika sherehe hizo, Rais Magufuli alisema viongozi wa serikali wanawategemea viongozi wa makanisa na misikiti katika kuwaongoza, ndiyo maana wanaheshimu mawaidha na mafundisho yao.
Alisema wao kama viongozi wa serikali, hawafurahii wanapoona makanisa na misikiti ikiwa na migogoro. Rais Magufuli alisema,“Ninapoona kuna migogoro ninajiuliza, ninapata shida nitakimbilia wapi.
Ukianza kusikia mahala pa uponyaji wa roho pana matatizo, ninaona roho za watanzania zitapotea. “Nishukuru kwa kumaliza mgogoro uliokuwepo hapa. Ni ushahidi wa kutosha kuwa kristo ameshinda na shetani ameshindwa.
“Askofu mteule mtangulize Mungu maliza makundi. Kuwa askofu wa makundi yote, usilipe kisasi waepuke watakaojipendekeza kwako kwa ushauri wa ajabu. Usilipize kisasi,” alisema Rais Magufuli.
Alisema, japo kusamehe ni jambo gumu lakini linawezekana hivyo, Anglikana wakisimama imara kwa kufuata maandiko ya kusameheana wataponya wengi. Magufuli alisema, kama kiongozi anapenda kuongoza watu waliosimama kiroho ili kusudi nchi iende vyema, kwani viongozi wa siasa kuongoza watu katika kanisa lililogawanyika linakuwa ni tatizo zaidi.
“Kama kiongozi wenu ninapenda kuongoza watu waliosimama kiroho ili kusudi nchi iende vyema. Naomba tatizo liishe kabisa lisitokee tena. Migogoro inaumiza zaidi wakristo, sisi viongozi wa siasa kuongoza watu waliogawanyika linakuwa tatizo zaidi.
“ Nimekuja hapa nikijua matatizo yaliyokuwepo hapa sasa yameisha. Hili lilitunyima nguvu, raha na tulimwezesha shetani kusimama. Lakini kwa haya yaliyotokea siku ya leo, shetani amelegea moja kwa moja,” alisema na kuwaasa wakristo wa kanisa hilo kuomba zaidi kwani shetani hajafurahi.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli alisema serikali ya awamu ya tano inashirikiana na madhehebu yote kuhakikisha ustawi wa watanzania unaenda mbele, na kwamba amepokea maombi yaliyotolewa na uongozi wa kanisa hilo atayafanyia kazi yale yatakayowezekana, yatakayoshindikana pia atawajulisha.
ASKOFU MKUU MSTAAFU
Awali Askofu Mkuu mstaafu wa kanisa anglikana tanzania, Donald Mtetemela alimuasa Askofu Jackson kuwa, kazi iliyopo mbele yake ni kubwa kwa kuwa inahusu roho za watu.
Pia alimueleza kuwa, asijiinue katika kazi ya Mungu kwani kwa kufanya hivyo atamaliza vibaya, kwani wote waliokwea ukuta akimaanisha waliopata nafasi za uongozi wa kiroho kwa njia isiyo halali wameumiza na kujeruhi kondoo wa Mungu.

Akizungumzia migogoro katika kanisa, alisema wao Anglikana walipita katika migogoro, na sababu kubwa ya mgogoro katika kanisa ni mali na vyeo. “Kanisa ni la Mungu halipaswi kuwa na mgogoro lakini kwa kuwa tunaishi duniani, shetani anajua ana muda mchache anautumia muda wake vibaya kuweka migogoro.
Mgogoro katika kanisa ni kazi ya shetani tusione ni halali bali ni chukizo,” alisema. Alisisitiza kuwa migogoro ni kazi ya shetani, viongozi wanaweza kuwa asili ya migogoro kwa sababu ya tamaa ya vyeo ama mali.
Alitoa angalizo pia kuwa migogoro hiyo haihusu kanisa la Anglikana pekee, kwani walipoguswa wao, madhehebu yote yanayomkiri Yesu Kristo yaliguswa. “Mpendwa wangu, umeibuka katikati ya migogoro lakini ni njia ya shetani ya kudhoofisha.
Shetani anafanya hivyo kupiga viongozi, kuvunja nguvu za kiroho, kuingiza watu wasiofaa kuwa viongozi. Sisi tunataka kanisa la Kristo liwe na watu wanaomcha Mungu,” alisema.
Alisisitiza kuwa migogoro na roho ya kutosameheana huacha majeruhi katika kanisa. Alishauri kanisa likemee maovu na kusimamia uadilifu, kwani haliwezi kukemea maovu kama kashfa inaliandama.
Pia aliwaasa viongozi wenzake wa kanisa kuwa wakati mwingine wanafikiri kukemea maovu ni kusimama hadharani bali sio hivyo wanaweza kumfuata faragha kiongozi wa kiserikali anayekosea na kumwonya.
“Tuheshimu viongozi wetu, kama wana maovu tuwafuate kwa utaratibu,” alisema. Alimwambia askofu huyo mteule Jackson kuwa, kazi yake siyo nyepesi, inabidi awe na ngozi nene na atakayempa ngozi hiyo ni Mungu mwenyewe. “Mungu akusaidie Jackson akutie nguvu akupe neema ya kutosha na kukubariki. Sisi tutakuombea usiogope, usiogope, usiogope,” alisema.
ASKOFU MKUU
Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini, Jacob Chimeledya aliomba vyombo vinavyoratibu shughuli za dini viwe makini kwani wapo wanaotumia jina la Anglikana isivyo na kulichafua kanisa hilo.
Pia alimwomba rais Magufuli kuangalia muingiliano uliopo katika hospitali zao ambapo pia kumejengwa na hospitali za serikali, hali inayoonekana kama ni ya kiushindani kati ya serikali na kanisa.
Kwa upande wake askofu mteule, Jackson alishukuru kwa uteuzi huo na kuahidi kusimama katika zamu yake. Pia alimwomba rais Magufuli, kama itawezekana serikali iwarudishie shule yao ya sekondari ya Minaki, na kutatua changamoto ya umeme katika hospitali zao.
Katika ibada hiyo viongozi waliohudhuria ni rais Magufuli na mkewe Janeth, rais mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe Anna, waziri mkuu mstaafu Jaji Sinde Joseph Warioba, Jaji Mkuu mstaafu, Agustino Ramadhan, naibu spika wa bunge Tulia Akson, waziri wa sheria na katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika.
Mapema mwaka jana, Askofu Mkuu wa kanisa hilo Chimeledya aliandika barua ya kumtaka askofu 

No comments