Header Ads

Rais John Magufuli amezindua Kituo cha Mafunzo Maalumu ya Kijeshi

Rais John Magufuli amezindua Kituo cha Mafunzo Maalumu ya Kijeshi
Rais John Magufuli akivuta utepe kufungua Kituo cha Mafunzo Maalumu ya Kijeshi kilichopo Mapinga, Bagamoyo mkoani Pwani jana. Wa Pili kushoto ni Naibu Mkuu wa Idara ya Usimamizi wa Mafunzo kutoka Tume Kuu ya Kijeshi ya China, Meja Jenerali Yang Jian na wa kwanza kushoto ni Balozi wa China hapa nchini Wang Ke. (Picha na Ikulu).

Rais John Magufuli amezindua Kituo cha Mafunzo Maalumu ya Kijeshi kilichopo Mapinga katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Kituo hicho kimejengwa kwa msaada kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China kwa gharama ya Sh bilioni 67.87 na kitatumika kutoa mafunzo ya kijeshi ya kisasa yatakayowawezesha askari kukabiliana na vitisho vya kisasa vya kiusalama.
Kabla ya kuzindua kituo hicho, Rais Magufuli na Balozi wa China nchini Wang Ke, walishuhudia makabidhiano ya kituo hicho kutoka Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa China lililowakilishwa na Naibu Mkuu wa Idara ya Mafunzo na Utawala ya Kamisheni Kuu ya Jeshi hilo Jenerali Yang Jian kwenda kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililowakilishwa na Meja Jenerali Yakub Hassan Mohamed.
Rais Magufuli pia alishuhudia mazoezi ya kijeshi yaliyofanywa katika kituo hicho yakiwemo shambulizi la kutokea baharini , makomandoo kukabiliana na magaidi na kupiga shabaha kwa kutumia miundombinu ya kisasa.
Akizungumza na maofisa, askari na wananchi waliojitokeza kushuhudia tukio la makabidhiano ya kituo hicho Rais Magufuli alilishukuru Jeshi la Ukombozi la Watu wa China na Serikali ya China kwa kutoa msaada wa kujengwa kwa kituo hicho na alisema Serikali ya Awamu ya Tano inathamini na kutambua mchango wa China katika Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania.
Alisema, China imeendelea kudhihirisha urafiki na udugu wake na Tanzania kwani licha ya kujenga kituo hicho pia imetoa msaada wa kujenga kituo cha mafunzo ya kijeshi ya anga cha Ngerengere mkoani Morogoro na miradi mingine ya maendeleo ya jamii na hivyo amemuomba Balozi Wang Ke kufikisha shukrani zake kwa Rais wa China Xi Jinping.
Balozi Wang Ke na Jenerali Yang Jian walisema China imejenga kituo hicho cha mafunzo maalumu ya kijeshi ambacho ni alama nyingine ya uhusiano na ushirikiano wa kirafiki na kidugu kati yake na Tanzania na wameipongeza JWTZ kwa kupata kituo ambacho wanaamini kitatumika kuimarisha ulinzi na usalama wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Mabeyo alisema, miundo ya kituo hicho inakifanya kuwa kituo cha kimataifa kilicho bora zaidi Afrika Mashariki na Kati kitakachoweza kutoa mafunzo ya kisasa kwa askari wengi na alimuomba Rais Magufuli kusaidia ujenzi wa daraja la mto Mpigi litakalokiunganisha na barabara ya kwenda Dar es Salaam.
Rais Magufuli pia amekubali maombi ya Jenerali Mabeyo ya kupeleka maji, umeme na barabara katika eneo ambalo China imekubali kutoa msaada wa kujenga makao makuu ya JWTZ

No comments