MAHAKAMA ya Hakimu mkazi Dodoma leo imemfutia kesi na kumuachia huru aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM)
MAHAKAMA ya Hakimu mkazi Dodoma leo imemfutia kesi na kumuachia huru aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM), Sadifa Juma Khamis, aliyekuwa akikabiliwa na makosa mawili yanayohusu rushwa baada ya upande wa Jamhuri kusema hauna nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Donge alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 11, mwaka jana kujibu tuhuma za makosa yanayohusiana na rushwa. Katika chumba cha Mahakama leo asubuhi, baada ya mshitakiwa na mawakili kuingia Mahakamani, Mwendesha mashtaka wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) Biswaro Biswaro aliiambia Mahakama kuwa kesi hiyo ilikuwa inakuja kwa ajili ya kutajwa lakini upande wa mashtaka unataka kuondoa shauri hilo mahakamani chini ya kifungu namba 98 (a) cha Mwendendo wa makosa ya jinai.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Joseph Fovo anayesikiliza kesi hiyo alimuuliza wakili upande wa utetezi, Godfyey Wasonga kama ana pingamizi lololote ambaye alijibu kuwa hana pingamizi. Hakimu Fovo alisema kutokana na maombi ya upande wa mashtaka, mahakamaa inaliondoa shauri hilo mahakamani chini ya kifungu namba 98(a) cha mwenendo wa makosa ya jinai. “Kesi hii inafutwa mahakamani lakini chini ya kifungu hiki hakizuii mshtakiwa kukamatwa na na kushtakiwa tena na Jamhuri kama watakuwa nauwezo wa kufanya hivyo,” alisema hakimu Fovo. Akizungumza nje ya mahakama kuhusiana na uamuzi huo, Sadifa alisema mahakama ni chombo kinachotoa haki na kweli haki imetendeka.
Post a Comment