Header Ads

MAMLAKA ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, imebainisha kutambua mtandano wa wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya


Image result for Wauza dawa za kulevya waanza kukimbia nchi
MAMLAKA ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, imebainisha kutambua mtandano wa wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya na kazi inayofuata sasa ni kuuvunja mtandano huo ulioko ndani na nje ya nchini, huku ikisema baadhi ya wahusika wameanza kutoroka nchini.
Aidha, Serikali imejipanga kushirikiana na Wizara ya Afya katika kudhibiti matumizi ya dawa zinazoruhusiwa kutibu za Valium, pethidine, dawa ya unga ya Morphine, Ketamine na Tramadol, ambazo kwa sasa zimeanza kutumika kama dawa za kulevya mbadala.
Pia Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya imesema itapima ugoro, unaotumiwa wa watumia dawa za kulevya, kama una kiwango cha Nicotine iliyoko kwenye tumbaku au la.
Hayo yalibainishwa jana na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Rogers Siyanga, mjini hapa jana wakati wa mkutano wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mku, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenister Mhagama aliyekuwa akizungumzia hali ya mapambano ya dawa za kulevya.
Alisema baada ya kubaini tabia, mienendo na mtandano wao, wamekuwa na kazi ya kuvunja mitandao hiyo, ikiwa ni kuwasaka wanaofanya biashara hizo ndani na nje ya nchi na kuwa tayari kuna waliokamatwa ambao walikuwa wamekimbia nchi.
“Ukiangalia mamlaka haina muda mrefu, tulichokuwa tunafanya ni kuwajua watu hawa na mitandano ya ndani na nje ya nchini na tunachofanya ni kuvunja mtandao wao na tunawafuata huko huku,” alisema Siyanga na kubainisha kuwa Watanzania wengi wamekimbilia Msumbiji na Afrika Kusini.
Kuhusu mikakati ya mamlaka, Siyanga alisema kati ya Januari na Februali mwaka huu, zimekamatwa kilo 1,365 ya dawa za kulevya katika kina kirefu cha bahari, ambazo zote zilikuwa zikiletwa nchini. Alisema kati ya dawa hizo, kilo 965 zilikamatwa na Meli Vita ya Jeshi la Australia (Combine Marine Forces) na kilo 400 zilikamatwa wiki iliyopita.
“Katika kipindi cha Februali, Meli Vita ya Jeshi la Australia, imekamata kilo 965 za dawa za kulevya ambapo kati ya kilo hizo 650 zilikuwa zikiingia Tanzania. “Pia katika kipindi hicho meli hiyo pia imekamata kilo 400 za dawa za kulevya ambazo haijafahamika zilikuwa zikipelekwa nchi gani,” alieleza.
Aidha Siyanga alisema kilo 200 za dawa za kulevya aina ya Heroine, zilikamatwa kwenye mpaka kati ya Msumbiji na Afrika Kusini, zikiwa zinasafirishwa kwenye gari linalomilikiwa na Mtanzania ambaye amekimbilia Afrika Kusini.
Kuhusu matumizi ya ugoro, ambao kwa sasa umeshika kasi kwa vijana kuutumia kutokana na udhibiti wa dawa za kulevya, alisema mamlaka hiyo itafanya utafiti kubaini kiwango cha “Nicotine” kilichopo.
“Inavyofahamika unapozungumzia ugoro maana yake ni matumizi ya tumbaku, lakini tumbaku inayotumika kwenye sigala ina kiwango cha kemikali ya Nicotine asilimia 14, sasa kwenye ugoro bado haifahamiki kiasi cha kemikali hiyo kilichopo.
“Mamlaka itafanya utafiti kubaini ni kiwango gani kilichopo na tutawatangazia wananchi.” Akielezea namna udhibiti unavyofanyika kwenye dawa za hospitali zinazotumiwa na watumiaji wa dawa za kulevya, Kamishna huyo alieleza taarifa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD), zinaonesha kuongezeka mahitaji ya dawa hizo.
Siyanga alisema Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na MSD, itaanza utafiti kubaini sababu za kuongezeka kwa mahitaji na namna ya kudhibiti. Kwa upande wake, Jenister alisema ukamataji dhidi ya wanaojihusisha na biashara hiyo, uko palepale.
Alisema mbinu mpya za ukamataji, zimeongezeka mara baada ya watumishi wa Mamlaka hiyo kumaliza mafunzo yao nje ya nchi pamoja na kukiimarisha kitengo cha Intelijensia. “Tutawafikia popote walipo.
Hatuchagui mtu wala cheo chake. Mapambano yanaendelea,” alisisitiza waziri huyo. Alisema mara baada ya kutungwa kwa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Mamlaka hiyo imekuwa chombo madhubuti, ambapo sasa kina uwezo wa kukamata na kudhibiti mali za wanaojihusisha na biashara hiyo.
Alisema licha ya mafanikio hayo, changamoto iliyopo ni ukubwa wa mpaka wa bahari ya nchi na wafanyabiashara kubadili mbinu za upitishaji wa dawa hizo. Pia alieleza wafanyabiashara wa dawa hizo, wamekuwa wakitumia kemikali bashirifu kutengenezea dawa za kulevya.
Waziri huyo alitaja magonjwa yanayowakabili watumiaji wa dawa za kulevya kuwa ni maambukizi ya virusi vya Ukimwi hususani kwa wanaochangia sindano kwenye kujidunga na homa ya ini.
“Tanzania kuna watumiaji 30,000 wa dawa za kulevya wanaojidunga kwa sindano ambao kati ya asilimia 34 hadi 42 wameathirika na Ukimwi. “Kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa watumiaji hao ni asilimia 11 wakati kiwango cha kitaifa cha ugonjwa wa kifua kikuu ni asilimia 0.2,” alifafanua.
Peter Mfisi ambaye ni Kamishna wa Kinga na Tiba kwenye Mamlaka hiyo, alisema taasisi zisizokuwa za kiserikali, zimekuwa zikitoa taarifa kuongezeka kwa waathirika wa dawa za kulevya wanaohitaji tiba.
Alisema moja ya taasisi hizo, ilieleza kuwa ilikuwa ikipokea maombi ya waathirika kwa wastani watu 20, lakini Desemba mwaka jana ilieleza kupokea maombi ya watu 50. Alisema mamlaka hiyo imeanza kufanya msako kwenye maduka ya dawa kubaini kama dawa za matibabu zinazotumiwa na watumiaji wa dawa za kulevya, zinauzwa kiholela.
Alieleza kuwa utoaji wa dawa hizo ni kwa wagonjwa pekee na hadi ambapo daktari atakapotoa mapendekezo.

No comments