Header Ads

TANZANIA imefanikiwa kuwatengeneza wadudu maalumu aina ya ‘Mexican Beetles,





TANZANIA imefanikiwa kuwatengeneza wadudu maalumu aina ya ‘Mexican Beetles,’ambao wameanza kutumika katika kuyatafuna majani hatari maarufu kama ‘magugu karoti’.
Majani hayo yamekuwa yakisambaa nchini tangu mwaka 2015 na kutishia afya za binadamu, mifugo na mazao shambani. Mtaalamu kutoka kitengo cha Sayansi ya Mimea kwenye Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (TPRI), jijini hapa, Ramadhan Kilewa alisema kuwa wadudu hao walizalishwa na kufanyiwa utafiti katika maabara za TPRI zilizopo Ngaramtoni, Arusha.
Alisema wameridhika kuwa wanaweza kuyaharibu majani hayo yenye sumu hatari kwa afya za wanadamu, wanyama na hata mimea shambani. “Tuliagiza mbegu kutoka Afrika Kusini na tumeanza kuwazalisha kwa wingi kwenye maabara zetu zilizopo Ngaramtoni na sasa tumeanza kuwapeleka wadudu hao kwenye maeneo ambayo ‘Magugu Karoti,’ hupatikana hapa Arusha, Manyara, Kilimanjaro na hivi karibuni pia yameonekana maeneo ya Kagera,” alisema.
Alisema wadudu hao hula magugu ya karoti peke yake, hawagusi mimea mingine na pale magugu hayo yenye sumu yatakapoisha kabisa basi hao wadudu nao wanakufa. Kaimu Mkurugenzi wa TPRI, Dk Margaret Mollel, pamoja na mratibu wa programu ya kudhibiti magugu karoti nchini, Dk Andrew Samora kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, Morogoro waliongoza upandikizaji wa wadudu hao katika mashamba yaliyoko kwenye vijiji vya Bwawani, Kazamoyo, Majengo, Lamolok na Mapinu katika kata ya Nduruma wilayani Arumeru.
Wakazi wa vijiji hivyo wamesema kuwa baadhi yao wamekuwa wakiathirika na sumu kutoka kwenye mimea hiyo; “Sisi huku tunaiita hii migugu karoti kuwa ni zao la kigaidi, tukiamini kuna mtu au watu walileta nchini ili kuharibu mimea na kudhuru binadamu na huu ni ugaidi,” alisema Mtendaji wa Kijiji cha Bwawani, Fred Kasale.
Taasisi hizo ni pamoja na ile ya utafiti wa madawa na kemikali za kilimo (TPRI), Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) na Shirika la ya Elimu kuhusiana na Ukame, Njaa na Mazao (ECHO), zote zikiwa na makao yao makuu jijini Arusha.
Miaka miwili iliyopita, Mtafiti Hannah Hacker, mtaalamu wa sayansi ya baiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Wheaton, Illinois Marekani ambaye anashiriki kwenye utafiti kwa niaba ya ECHO, aliwahi kukiri kuwa mmea huo unaua.

No comments