MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha St Augustine (SAUT) anashikiliwa na Jeshi la Polisi
MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha St Augustine (SAUT) Tawi la Mbeya na wenzake wawili, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukamatwa wakiwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh milioni 33.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohamed Mpinga aliwataja watu wanaowashikilia kuwa ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha SAUT, Kenedy Simsokwe (43), mpiga picha Mathew Mwanjala (42) wote wakazi wa Iyela na Shabani Mkwiche (24) mkazi wa Iyunga katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Akizungumzia tukio hilo, alisema kuwa Februari 5, mwaka huu polisi wakiwa katika majukumu yao ya kawaida ya kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao watatu wakiwa na nyara hizo za serikali kinyume cha sheria.
Mpinga alisema baada ya kuwakamata na kuwapekua walikutwa wakiwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo tano vikiwa na thamani ya Sh milioni 33, ambapo alisema taratibu za kisheria zinafanyika ili watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani kwa hatua zaidi.
Aliwataka wananchi wenye taarifa za mtu au kikundi cha watu kinachojihusisha na ujangili, watoe taarifa katika vyombo husika ili hatua zichukuliwe ili kuweza kudhibiti vitendo hivyo, ambavyo vimekuwa vikiliingizia Taifa hasara na kutishia kutoweka kwa baadhi ya wanyama ambao wanawindwa zaidi na majangili.
Aliwataka wananchi na hasa vijana, kuacha tamaa ya kupata fedha nyingi kwa njia ya mkato, jambo linalosababisha wajiingize katika matendo maovu, badala yake watumie njia halali katika kupata fedha kwa manufaa ya kwao, familia na Taifa.
Post a Comment