Mke aua mume kwa shoka kisha kujimaliza
Mke aua mume kwa shoka kisha kujimaliza
WATU wawili, mume na mke, wakazi wa kijiji cha Igosi wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe, wamekufa usiku wa kuamkia jana, mmoja wa kukatwa na shoka mna mwingine kwa kujinyonga.
Katika tukio hilo mke alimpiga shoka mumewe kichwani, kisha na yeye kujinyonga kwa kamba.
Mrakibu Mwandamizi Mfawidhi wa Polisi Mkoa wa Njombe, John Temu, amethibitisha kutokea kwa matukio hayo na amemtaja aliyejinyonga kuwa ni Ajenta Nziku.
Alijinyonga kwa kamba ya katani sebuleni kwake, baada ya kumuua mumewe, Ludoviki Mgaya aliyekutwa amekufa chumbani kwake.
Kamanda Temu amesema chanzo cha vifo hivyo inasadikika ni wivu wa mapenzi uliotokana na Ludoviki kuoa mke wa pili, kitendo ambacho hakikumfurahisha mkewe mkubwa, hivyo kuamua kuchukua sheria mkononi ya kumuua kwa shoka.
Amesema, baada ya kuua, Ajenta naye aliamua kujinyonga kwa kamba ya katani.
Alisema jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi kubaini sababu za tukio hilo.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Igosi, Pascal Mpumbi alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa sita na saa saba usiku.
Amesema, alipigiwa simu na majirani na alipofika eneo la tukio, alishuhudia wanandoa hao wakiwa wamelala chini na papo hapo alitoa taarifa polisi.
Msemaji wa familia ya akina Mgaya, Abel Mgaya ambaye ni baba mdogo wa Ludoviki, alisema chanzo cha vifo hivyo ni wivu wa mapenzi uliosababishwa na mtoto wao kuoa mke wa pili.
Alisema wao kama familia, waliwahi kusuluhisha na baadaye kwenda ofisi ya kata, ambako walimaliza suala hilo.
Post a Comment