Majeshi yanayoongozwa na Marekani katika kupambana na makundi ya itikadi kali yamefanya mashambulizi ya anga
Majeshi yanayoongozwa na Marekani katika kupambana na makundi ya itikadi kali yamefanya mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vinavyomuunga mkono rais wa Syria Bashar al Assad.
Muungano wa majeshi yanayoongozwa na Marekani katika kupambana na makundi ya itikadi kali umefanya mashambulizi ya anga dhidi ya vikosi vinavyomuunga mkono rais wa Syria Bashar al Assad na kuwaua zaidi ya wapiganaji 100 wa vikosi vya serikali. Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la Marekani. Isaac Gamba anaarifu zaidi katika taarifa ifuatayo.
Mashambulizi hayo ya anga yalikuwa yanalenga kujibu shambulizi lilofanywa katika makao makuu ya vikosi washirika na Marekani vya Syrian Demokrasia Forces (SDF) ambavyo vimekuwa vikitoa mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiisilamu ( IS ).
Afisa mmoja wa jeshi la Marekani amesema wanakisia kuwa zaidi ya wapiganaji 100 wa vikosi vinavyounga mkono utawala wa Syria wameuawa wakati wa mapambano hayo ambapo pia mpiganaji mmoja wa vikosi vya SDF aliuawa.
Shambulizi lilihusisha wapiganaji 500
Hata hivyo afisa huyo wa jeshi la Marekani hakufafanua zaidi iwapo vikosi ambavyo vilikuwa vinapambana na muungano na majeshi yanayoongozwa na Marekani vilikuwa ni vya serikali ya Syria au vya makundi kadhaa ya wanamgambo washirika yakiwemo kutoka Iraq na Lebanon ambayo yamekuwa yakimuunga mkono rais Assad tangu mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalipozuka nchini Syria miaka saba iliyopita.Amesema shambulizi hilo lililoanza jana Jumatano lilihusisha wapiganaji 500 wa vikosi vinavyoiunga mkono serikali ya Syria vilivyokuwa vikitumia vifaru na silaha nyingine katika mapambano hayo.
Urusi nayo pia imekuwa ikifanya mashambulizi ya anga nchini humo kumuunga mkono rais Bashar Assad ambaye pia amekuwa akisaidiwa na Iran.
Kundi la waasi wa SDF ambao ni muungano wa vikosi vya Kikurdi na wapiganaji wa kiarabu linashirikiana na vikosi vya muungano unaooongozwa na Marekani kuwasambaratisha kabisa wanamgambo wa kundi la itikadi linalojiita Dola la Kiisilamu waliosalia katika ukingo wa mashariki wa mto Euphrates baada ya vikosi hivyo kufanikiwa kudhibiti ngome kuu ya kundi la IS ya Raqa.
Shambulizi hilo linaweza kusababisha changamoto zaidi kwa wapiganaji wa vikosi vinavyoungwa mkono na Marekani ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakijaribu kuzuia makabiliano na vikosi vinavyoiunga mkono serikali ya rais Bashar Assad.
Wakati huohuo kwa mjibu wa Ikulu ya Urusi Kremlin rais Vladimir Putin na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye operesheni za kijeshi na kiusalama nchini Syria katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Katika mazungumzo yao kwa njia ya simu rais Putin na Erdogan walijadili pia juu ya kuwa na mawasiliano mapya yatakayoijumuisha pia Iran kujadili mgogoro huo wa Syria na kwa mujibu wa Kremlin viongozi hao pia walijadili juu ya haja ya kufanyika mkutano huo wa kilele kati ya viongozi wa nchi hizo tatu ingawa tarehe haijapangwa.
Post a Comment