Header Ads

RAIS Salva Kiir amewaomba wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kusaidia kupatikana kwa amani




RAIS Salva Kiir amewaomba wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kusaidia kupatikana kwa amani ya kudumu latika taifa hilo na nchi nyingine za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kiongozi huyo wa Sudan Kusini ametoa ombi hilo wakati wa mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi za EAC jijini Kampala, Uganda.
Ametumia nafasi hiyo kuwaomba rasmi viongozi wa EAC kuongeza juhudi zao za amani ya kudumu katika nchi za Sudan Kusini, Burundi na DRC, akisisitiza vita na migogoro ya mara kwa mara inachangia kurudisha nyuma maendeleo ya ukanda wa jumuiya hiyo yenye nchi sita ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.
Aligusia pia umuhimu wa EAC kuiunga mkono Sudan Kusini ili ichangie maendeleo katika sekta za miundombinu, afya na nyinginezo ndani ya jumuiya.
Mwenyekiti wa EAC, Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliwataka wakuu wengine wa nchi za jumuiya hiyo kuwaunganisha raia wake zaidi ya milioni 160 na miradi ya uwekezaji wa ndani katika miundombinu ili kukuza tija katika uzalishaji na mengineyo.
“Wakati maeneo mengine ya Afrika yakitambaa kimaendeleo, Ukanda wa Afrika Mashariki unakua kwa kasi. Kwa kiasi fulani, hii ni kwa sababu ya kuimarika kwa mawasiliano na kuimarisha miundombinu,” alisema. Museveni amezitaka pia nchi kukabiliana na changamoto za kibiashara ili thamani ya fedha katika uwekezaji wa miundombinu ionekane.
Wakati huohuo, Waziri anayeshughulikia nishati ya Petroli Sudan Kusini, Ezekiel Gatkouth amepinga pendekezo la kumtaka Rais Kiir aachie ngazi ili kupisha mchakato wa amani nchini hapa ikiwa ni pamoja na kuandaa uchaguzi mkuu.
Aliyasema hayo jijini hapa wakati wa mkutano ulioshirikisha wadau wa mafuta na umeme. “Kwa sisi wengine, tunataka aendelee, Makamu wa Kwanza wa Rais, Taban Deng Gai aendelee, Makamu wa Rais, James Wani aendelee… tutapanua wigo wa uongozi katika kuhakikisha malengo yetu ya kupata amani yanatimia,” alisema Gatkuoth.
Kiongozi huyo wa zamani wa waasi aliyegeuka kipenzi cha Serikali na kuteuliwa kuwa Waziri mwaka 2016 baada ya kuondoka madarakani kwa Makamu wa Rais, Riek Machar, anasema ni vyema kila mmoja, bila kujali ni adui au la, akapewa nafasi ya kushirikiana kutafuta amani ya kweli ya Sudan Kusini, badala ya kubaguana.
Uongozi wa SPLM-IO unaoongozwa na Taban Deng Gai na Rais Kiir mwenyewe, unapinga ushiriki wa Makamu wa Rais wa zamani, Machar katika Serikali ya muda wakiamini anaweza kuwavuruga.
Hata hivyo, wafuasi wa Machar anayeishi uhamishoni Afrika Kusini hawajawekewa pingamizi. Waziri Gatkuoth amesema katika mji anaotoka wa Upper Nile, raia waliokimbia machafuko wameanza kurejea nyumba, akifafanua kuwa waliorejea ni wastani ya asilimia 90 ya watu waliokuwa wamekimbia.
“Watu wameitikia vyema mwito wa kurejea nyumba. Wanarejea na kuimarisha amani nchini baada ya kuridhishwa na hali ya amani ilivyo sasa. Wanarejea kuja kuijenga nchi,” alisema Gatkuoth.
Wakati wa kuanza kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe Desemba mwaka 2013, alikuwa mfungwa wa zamani wa kisiasa, alipoachiwa alijiunga na waasi wa Machar kabla ya kujiengua na kuungana na upande wa Taban Deng Gai.

No comments