Header Ads

RAIS John Magufuli amesema, amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwanasiasa


Image result for kingunge

RAIS John Magufuli amesema, amepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwanasiasa mkongwe nchini Kingunge Ngombale Mwiru.
Mwanasiasa huyo mkongwe aliyelitumikia Taifa kwa uzalendo na uadilifu, alifariki jana alfajiri katika hospitali ya taifa ya Muhimbili , anatarajiwa kuzikwa Februari 5, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Rais alisema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kupigania uhuru na baada ya kupata uhuru akiwa mtumishi mtiifu wa chama cha TANU na baadaye CCM, na katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya serikali.
“Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka, ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu,” alisema Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Balozi Juma Mwapachu, alisema Kingunge atakumbukwa kwa mambo mengi kwani alikuwa ni kiongozi shupavu ambaye alifanya kazi kwa karibu na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Huu ni msiba wa Watanzania wote kwa sababu mzee huyu ni mwanasiasa mkongwe na mimi nikimfahamu toka mwaka 1967 katika siasa hizi alikuwa mpambanaji,” alisema Balozi Mwapachu. Kingunge alifariki jana alfajiri wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam baada ya kushambuliwa na mbwa wake nyumbani kwake Victoria, Dar es Salaam mwezi mmoja uliopita.

No comments