Ujenzi wa njia sita Dar -Kiluvya kumalizika hivi karibuni
Ujenzi wa njia sita Dar -Kiluvya kumalizika hivi karibuni
RAIS John Magufuli amesema upanuzi wa barabara ya Morogoro wa njia sita kutoka Kimara jijini Dar es Salaam hadi Kiluvya wilayani Kinondoni, karibu na Kibaha mkoani Pwani, sasa utaanza mwezi huu.
Alisema hayo jana akizindua pasipoti mpya za kusafiria za kielektroniki za Tanzania, Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji nchini jijini Dar es Salaam. Alisema upanuzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 16, utapunguza changamoto ya msongamano wa magari. Dk Magufuli aliwahakikishia wananchi wa Dar es Salaam kuwa serikali imejipanga kuwatetea na kutatua shida zao.
Alisema anafahamu moja ya kero kubwa Dar es Salaam ni msongamano wa magari, ambayo ameshaanza kuichukulia hatua.Katika kukabiliana na kero, Rais Magufuli alisema mbali na upanuzi wa barabara ya Morogoro, awamu ya pili ya ujenzi wa barabara ya mabasi ya mwendo kasi kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwenda Mbagala, nao utaanza mwaka huu.
“Tunajenga madaraja ya juu pale Tazara na Ubungo ambayo yote yatagharimu takriban Shilingi bilioni 300,” alieleza. Aidha alisema ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma, nao umeshaanza.
Alisema reli hiyo ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, yenye urefu wa kilomita 712 itagharimu Sh trilioni 7.06, ambazo zote ni fedha za Serikali. Alisema reli inayoelekea mikoa ya Mwanza na Kigoma, ambayo pia itaunganishwa na reli ya kwenda nchi za Burundi na Rwanda, itarahisisha usafiri kati ya Dar es Salaam na Makao Makuu ya nchi, Dodoma, ikiisha. Rais alisema Serikali inaboresha huduma za jamii ikiwemo maji, afya na elimu.
Post a Comment