Wakimbia hospitali kuhofia kulazwa na maiti
UKOSEKANA kwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Mtowisa wilayani Sumbawanga, kumesababisha maiti kuhifadhiwa wodini pamoja na wagonjwa waliolazwa humo kwa matibabu.
Taarifa zilizopo zinadai kuwa wagonjwa waliolazwa katika kituo hicho cha afya, wamekuwa wakitoroka na kurejea kwao baada ya miili hiyo ya marehemu kuhifadhiwa humo kwa siku mbili mfululizo na kuanza kuharibika, ikisubiri kuchukuliwa na ndugu zao kwa maandalizi ya maziko. Hayo yalibainika baada ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo aliyetembelea jana kituoni hapo.
“Zipo taarifa za uhakika kuwa wagonjwa wanakimbia wodini walimolazwa na kurejea makwao wakiwa bado wanapatiwa matibabu, wakihofia kulala chumba kimoja maiti wanaohifadhiwa wodini kutokana na ukosefu wa chumba cha kuhifadhia maiti. Wagonjwa wanakimbia na kurejea makwao kwa hofu ya kuchangia wodi moja na maiti inayohifadhiwa humo. Sisi binadamu ni hulka yetu mwenzetu anapokufa sio rafiki tena anakimbiwa hata na nduguze,” alieleza Wangapo, akihutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Mtowisa.
Alimuagiza Diwani wa Kata ya Mtowisa, Edgar Malinyi awahamasishe wananchi wake waanze kujenga chumba cha maiti. Alisisitiza kuwa atakaporudi Juni, mwaka huu, atatoa mabati ya kuezeka kumalizia ujenzi . Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtowisa A, Didas Malingumu alikiri kukosekana kwa chumba cha maiti katika kituo hicho cha afya. Alisema suala hilo ni kilio chao cha muda mrefu .
“Kutokana na hali ya joto kali, miili inayohifadhiwa wodini pamoja na wagonjwa imekuwa ikiharibika muda mfupi tu na kusababisha taharuki kubwa kwa wagonjwa, ambao wanalazimika kukimbia na kurejea nyumbani,” alisema. Chumba cha maiti cha karibu na kata hiyo kiko Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga, umbali wa kilometa 100.
MARUFUKU YA BANGI KUTO LEWA
Post a Comment