Header Ads

ufa walioghushi vyeti kuzibwa


SERIKALI imebainisha kuwa kati ya watumishi 14,000 waliogundulika kuwa wamejipatia kazi kwa kughushi vyeti vya taaluma, 3,310 walitokea Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.
Hata hivyo, imesema sasa imeanza mchakato wa ajira mpya ambapo kwa mwaka 2017/18 na 2018/19 inatarajia kuajiri watumishi wapya zaidi ya 100,000, kati yao 14,104 sawa na asilimia 26.6 ni wa kada ya afya.
Hayo yamesemwa bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, wakati wa kuhitimishwa mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Mkuchika amesema kuanzia Oktoba, 2016, serikali ilifanya uhakiki wa watumishi wa umma na walipatikana watu 14,000 waliojipatia kazi kwa kughushi ambao 3,310 walitokea Wizara ya Afya.
"Serikali ilisitisha ajira baada ya kujiridhisha. Uhakiki huu sasa umekamilika na kazi inayofanywa na wizara ni kuziba pengo la watu walioondoka kwenye utumishi wa umma,” amesema Mkuchika.
Amesema katika mwaka wa fedha wa 2017/18, serikali iliajiri watumishi mbadala 2,500 na katika mwaka huohuo, kupitia bajeti ya Ofisi ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Bunge lilipitisha ajira 52,436 zikiwemo 14,104 sawa na asilimia 26.6 za watu wote wa kada ya afya.
Mkuchika amesema, katika bajeti ya mwaka 2018/19 ya Utumishi wa Umma ambayo tayari Bunge limeipitisha, watumishi wengine 49,536 wataajiriwa na hivyo ndani ya miaka hiyo, serikali itaajiri watumishi wapya zaidi ya 100,000.
Alieleza kuwa kupitia mchanganuo huo, kwa miaka hiyo miwili ya fedha watumishi wa kada ya afya watakaoajiriwa rasmi ni 16,205 sawa na asilimia 32.7 asilimia ya watumishi wote watakaoajiriwa.
"Msisitizo na lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa huduma ya afya nchini haikwami," alisema Mkuchika. Kutokana na hoja za wabunge waliodai kuwa kuna baadhi ya vituo vya afya na zahanati zilizofungwa kwa kukosa watumishi baada ya wengi kusitishiwa ajira baada ya kukutwa na vyeti feki, Mkuchika alisema serikali haitoruhusu kituo kifungwe kwa sababu ya ukosefu wa watumishi.
"Nilishatuma maagizo kwamba Serikali ya CCM haitaruhusu kituo kifungwe kwa sababu ya kukosa watumishi. Waheshimiwa wabunge nawahakikishia nikipata taarifa nitahamisha watu kutoka popote..."
"...Yeyote aliyeongea humu ndani (bungeni) na ana uhakika kuna zahanati au kituo cha afya kimefungwa, nilitewe taarifa wakati Bunge linaendelea nitapeleka watu," alisisitiza.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndungulile amesema serikali imekuwa ikiboresha vituo vya afya na zahanati mara kwa mara na kwa mujibu wa Sera ya Afya inaeleza kila kijiji na kila kata itakuwa na zahanati.
Alieleza kuwa bajeti ya mwaka 2018/19, imetenga fedha kujenga hospitali za wilaya 67 na hospitali sita za rufaa za mikoa.
"Tumeboresha huduma za afya pia, kwa kuanzisha mfumo wa uwekaji viwango vya ubora wa utoaji huduma. Tangu tuanze zaidi ya asilimia 33 ya vituo vya afya huduma zake zilipata alama ya sifuri. Lakini sasa kadri tunavyoendelea alama hizi zinaanza kupanda," amesema Dk Ndungulile.
Aidha, alisema serikali ina mpango wa kuanzisha utaratibu wa kutoa leseni kwa vyombo vinavyotoa huduma za afya itakayotolewa kwa mujibu wa viwango vya ubora vilivyopo.

sima itabali kwa simba angalia video

No comments