Header Ads

UJENZI wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) maarufu mwendo kasi kwenda Mbagala na Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, umepangwa kuanza mwaka huu.


UJENZI wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) maarufu mwendo kasi kwenda Mbagala na Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, umepangwa kuanza mwaka huu.
Aidha, usanifu wa ujenzi wa miundombinu ya Dart, utakaohusisha barabara za Sam Nujoma, Bagamoyo, Bibi Titi na Ali Hassan Mwinyi zenye urefu wa kilometa 25.9, pia unaanza mwaka huu wa fedha. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alisema hayo jana wakati akiwasilisha bungeni mapitio, makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Jafo katika kuzungumzia malengo ya taasisi zilizo chini ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2018/19 ikiwemo DART, alisema ujenzi huo utakwenda pamoja na utekelezaji mpango kazi wa fidia ya makazi kwa waathirika wa mradi wa awamu ya pili na tatu na kulipa fidia kwa ajili ya mradi wa awamu zote. Alisema ujenzi wa miundombinu hiyo ya Mbagala na Gongo la Mboto, umepangwa kuanza Desemba mwaka huu chini ya awamu ya pili na tatu. Ujenzi awamu ya pili (Mbagala) utahusisha barabara za Kilwa, Kawawa, Sokoine, Gerezani, Bandari na Chang’ombe zenye urefu wa kilometa 20.3 na ujenzi utaanza baada ya kumpata mkandarasi.
Mradi huo utatekelezwa kupitia mkopo wa dola za Marekani milioni 141.71 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika. Kwa upande wa awamu ya tatu ya ujenzi (kwenda Gongo la Mboto), utahusisha barabara za Nyerere, Uhuru, Bibi Titi, Azikiwe, Shaurimoyo, Lindi na Maktaba zenye urefu wa kilometa 23.6 kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 148.2 kutoka Benki ya Dunia.
Akizungumzia usanifu wa awamu ya nne ya ujenzi wa miundombinu hiyo ya Dart, Jafo alisema utafanyika kwa mkopo wa dola za Marekani milioni 97.9 kutoka Benki ya Dunia. Usanifu utahusisha barabara za Sam Nujoma, Bagamoyo, Bibi Titi na Ali Hassan Mwinyi zenye urefu wa kilometa 25.9. Malengo mengine ya DART ni ujenzi wa maegesho katika maeneo ya mfumo wa wakala; kukamilisha taratibu za upatikanaji wa mtoa huduma wa pili (SP2), mkusanyaji nauli, msimamizi wa fedha pamoja na mshauri mwelekezaji kwa ajili ya awamu ya tatu.
darasa la saba kudhaminiwa

No comments