Header Ads

Mapato Tanesco ya ongezeka hadi bilioni 32/-



KUANZIA Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu, mapato ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) yameongezeka kutoka Sh bilioni 29.1 hadi Sh bilioni 32.3.
Hata hivyo, pamoja na ongezeko hilo mapato, bado shirika hilo linakabiliwa na gharama kubwa ya uedeshaji, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya gharama zinazotokana na uzalishaji zinatokana na uzalishaji umeme, ukarabati mitambo na miundombinu muhimu ya umeme.
Hayo yalibainishwa bungeni Dodoma jana na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alipojibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Bulembo (CCM).
Mbunge huyo katika swali lake, alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kuondokana na gharama kubwa za uendeshaji wa shirika hilo kutokana gharama za uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta.
Lakini, pia alihoji ni lini shirika hilo litagawanywa ili liweze kutenganishwa kwenye uendeshaji na uzalishaji.
Akijibu swali hilo, Dk Kalemani alikiri kuwa shirika hilo bado linajiendesha kihasara, lakini sasa baada ya hatua zilizoanza kuchukuliwa na serikali, mapato ya shirika hilo yameanza kuongezeka.
"Sababu za mapato kuongezeka ni baada ya serikali kupiga marufuku kununua vifaa vya umeme kutoka nje ya nchi, kuachana na matumizi ya uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta na kufunga mfumo wa LUKU kwa wananchi wote wanaotumia umeme," alieleza Dk Kalemani.
Mbunge wa Magomeni, Jamal Kassim Ali (CCM) katika swali lake la msingi alitaka kujua serikali, ina mpango gani wa kulifanya Shirika hilo liweze kujiendesha kwa faida.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Subira Mgalu wakati akijibu swali hilo, alisema shirika hilo linakabiliwa na gharama kubwa za uendeshaji.
Zaidi ya asilimia 80 ya gharama, zinatokana na uzalishaji umeme, ukarabati wa mitambo na miundombinu mingine muhimu ya umeme.
Alisema mapato ya shirika yamekuwa hayakidhi vya kutosha gharama za uendeshaji hususan katika maeneo ya uzalishaji wa umeme, kwa kutumia mafuta mazito, ambayo ni ghali.
"Shirika linakabiliwa na tatizo la malimbikizo ya madeni ya wateja wakubwa, kawaida na wadogo kushindwa kulipa Ankara za umeme kwa wakati zikiwamo taasisi na mashirika ya umma pamoja na wateja wengine," alisema.
Alieleza kuwa kwa sasa serikali ina mikakati madhubuti ya kuliwezesha shirika hilo, kujiendesha kibiashara na kuondokana na hasara.
Alitaja mikakati hiyo kuwa ni kuongeza uzalishaji wa umeme, kwa kufanya uwekezaji katika mitambo ya kufua umeme, kwa kutumia gesi asilia na maji ili kuepukana na mitambo inayotumia mafuta.
Alisema tayari mipango inaendelea kuanza utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 2100 wa Rufiji (Stieglier's Gorge), utakaozalisha umeme kwa gharama nafuu, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uzalishaji wa umeme.
"Pia shirika lijiendeshe kibiashara, miradi mingine ni megawati 300 zitokanazo na gesi asilia eneo la Mtwara na megawati 330 katika eneo la Somangafungu mkoani Lindi,"alisema.
Alisema kwa kipindi cha karibuni, maeneo ya Kibiti, Ikwiriri na Ngara yameunganishwa katika Gridi ya Taifa, hivyo kupunguza gharama za uendeshaji zilizokuwa zikitokana na matumizi ya mafuta mazito.

ANGALIA HAPA CHINI SYLAS TV 


No comments