baraza huru la habari
VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuanza mchakato mara moja wa kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Habari ambalo litawatambua wanahabari kama wanataaluma, lakini pia kusimamia haki na maslahi yao.
Baada ya kuanza kutumika rasmi kwa Kanuni za Maudhui mitandaoni, redioni na kwenye runinga, tayari maombi 86 ya blogu, majukwaa ya kimtandao, redio na televisheni za mitandaoni zinazotaka kujisajili yametumwa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe aliyasema hayo bungeni Dodoma wakati akihitimisha hoja ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Dk Mwakyembe alisema kutokana na ukosefu wa chombo hicho ambacho kiko kwa mujibu wa Kanuni zilizo chini ya Sheria ya Huduma za Habari Namba 12 ya Mwaka 2016, kwa sasa kazi ya uandishi wa habari haitambuliki kama taaluma na wanahabari wengi wanafanya kazi kwa katika mazingira magumu kimaslahi.
“Watu wa kuwaonea huruma ni waandishi wa vyombo vya habari binafsi, kuna waandishi wanapata mshahara wa kitumwa yaani upo hata chini ya kiwango cha kima cha chini…”
“…Hakuna mkataba wa kazi, kwa kweli vijana wangu wanachezewa sana, hawawekewi hata bima wala kuingiziwa kwenye mifuko ya hifadhi. Undeni Media Council (Baraza la Habari) yenu tutawasaidia, chini ya sheria hii mtakuwa na ajira inayowalinda wengi,” amesisitiza.
Amesema katika majadiliano ya kupitisha bajeti hiyo, wabunge wengi ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, walihoji kwa nini mpaka sasa serikali haijaliunda baraza hilo wakati sheria na kanuni zilishatoka na kuanza kutumika.
Alisema pamoja na kwamba katika bajeti ya mwaka 2018/19 wizara yake imeomba fedha za uanzishwaji wa chombo hicho cha Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Habari, mchakato mzima wa uanzishwaji wake unavihusu zaidi vyombo vyenyewe vya habari.
“Kwa sababu serikali ikianzisha yenyewe, yataanza maneno kwamba chombo hiki hakiko huru, naomba vyombo vya habari vijitokeze tuunde hii bodi. Lengo kubwa la serikali ni hivi vyombo vijiendeshe vyenyewe,” alisema.
Akizungumzia kanuni mpya zilizo chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta ya mwaka 2010, alisema tayari watumiaji wa blogu, majukwaa ya mitandao, redio na televisheni za mitandaoni wameanza utekelezaji wa kanuni hizo na 86 wametuma maombi ya kusajiliwa.
Alisema sababu hasa za serikali kuanzisha kanuni hizo ni kutokana na ukweli kuwa vyombo hivyo, hivi sasa duniani vinabeba nafasi sawa na vyombo rasmi vya habari katika kuhabarisha.
“Naamini ndani ya miaka mitatu vitakuwa vikubwa kuliko vile rasmi. Redio na runinga za mitandaoni na majukwaa mitandaoni vimeanza kuwa muhimu katika kuhabarishana, tatizo havina utambulisho rasmi kwamba ni wanahabari, hawana miiko ya uandishi wa habari, hawabanwi na maadili yoyote, hawalipi kodi pamoja na kwamba wanashindana na vyombo rasmi hii si fair (haki),” alisisitiza.
Alisema kutokana na matumizi makubwa ya vyombo hivyo vya habari kupitia mitandaoni, siku hizi mtu anaweza asisome gazeti hata kwa wiki nzima, lakini akiendelea kupata habari zote kupitia majukwaa hayo ya mtandaoni, blogu, redio na runinga za mtandaoni.
Alieleza kuwa kuwekwa kwa kanuni hizo kunalenga kuvidhibiti vyombo hivyo kimaadili na kuvitambua kitaaluma kwa kuwa uendeshaji wake wa sasa una changamoto kubwa ya ukosefu wa maadili na miiko ya taaluma ya uandishi wa habari.
“Hivi vyombo vina changamoto kubwa, lazima viwe na maadili na miiko. Tatizo la vyombo vya mitandaoni vimejaa fake news, wapotoshaji na waongo. Kuna nchi zimekaribia kwenda vitani kwa ajili ya vyombo hivi,” alifafanua.
Alieleza kuwa asilimia 75 ya nchi duniani zimechukua hatua kudhibiti maudhui kwenye mitandao.
Alitaja baadhi ya nchi zilizoweka udhibiti wa maudhui ya mtandaoni kuwa ni Marekani, Australia, Uingereza, Canada na India ambapo sasa Tanzania nayo imeona wajibu wa kulinda maudhi hayo ya mitandao. Bunge liliidhinisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/19 ya Sh bilioni 33.3 ambapo kati ya fedha hizo mishahara ni Sh bilioni 12.2, matumizi mengine ni Sh bilioni 9.3 na miradi ya maendeleo ni Sh bilioni 8.7.
Post a Comment