Header Ads

Michepuko chanzo kuvunjika ndoa’



WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) umesema kuwa kwa miaka mitatu iliyopita talaka 330 zimetolewa, kisheria.
Mkurugenzi wa Masuala ya Haki na Ulinzi wa kisheria kutoka Rita, Lina Msanga alisema takwimu za usajili wa talaka inaonesha kuwa mwaka 2015 zilisajiliwa talaka 94, mwaka 2016 talaka 110 na mwaka jana talaka 126. Msanga alisema suala la wanandoa kuwa na michepuko imekuwa ni moja ya sababu kuu zinazosababisha ndoa nyingi kuvunjika. Kwa mujibu wa Msanga, ndoa nyingi hasa za miaka ya karibuni zinavunjika kutokana na aidha mume au mke kuwa na mchepuko, jambo linalosababisha kuwepo kwa talaka. “Ukiangalia takwimu zetu za kusajili talaka utaona kabisa kuwa kuna ongezeko la kasi hivyo ni muhimu kwa wanandoa kujitahidi kuwa waaminifu ili kulinda ndoa zao na familia kwa ujumla.
“Suala la kuvunjika kwa ndoa si zuri na linaweza kuathiri watoto hasa katika kujipatia mahitaji yao ya msingi kama elimu,” alisema. Aliongeza kuwa sababu nyinginezo ni watu kutofahamiana vizuri mpaka kuamua kufunga ndoa na kuanza kugundua tabia ambazo haziendani na kushindwa kuvumilia mwisho wa siku wanaachana. “Hii ni tofauti sana na enzi ya wazazi wetu ambapo wao walikuwa wakifanya uchunguzi wa kina kujua tabia na mpaka familia anayotokea mhusika ndipo ndoa ifungwe,” alisema.
Alisema iwapo wanandoa wataamua kuachana basi ni vizuri wafuate utaratibu wa kusajili talaka zao katika ofisi za Rita ili kuwezesha kupata hati ya talaka ambayo ni uthibitisho wa hali ya ndoa husika, lakini pia itasaidia kulinda mali ya mtalaka endapo atafariki na mtalikiwa kudai urithi wake. “Mwombaji wa talaka anatakiwa kupeleka malalamiko yake kwenye Baraza la Usuluhishi la Ndoa linalotambuliwa kisheria kisha atapewa hati maalumu ambayo ataipeleka mahakamani na kulifungua shauri la kuomba ndoa hiyo ivunjwe kisheria ambapo mahakama ikiridhia itatoa tamko la kuvunjika kwa ndoa. “Na tamko hilo litawasilishwa Rita kwa Msajili Mkuu wa Ndoa na talaka ili kusajili,” alisema Msanga.

NANDI AKANA KUCHEPUKA NA BILINAS


No comments