Header Ads

HISTORIA mpya imeandikwa Tanzania


Rais John Magufuli akifunua pazia kuzindua ukuta wenye urefu wa kilomita 24.5 kuzunguka eneo la mgodi wa madini ya Tanzanite lililopo Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara jana. Kulia kwake ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Mabeyo, mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli (kushoto) na viongozi wengine wa kiserikali.
HISTORIA imeandikwa Tanzania baada ya Rais John Magufuli kuzindua ukuta unaozunguka eneo lote la madini ya tanzanite, Mirerani wilayani Simanjiro, yakiwa ni madini yanayopatikana Tanzania pekee.
Ukuta huo wenye urefu wa kilometa 24.5, uliogharimu Sh bilioni 5.6, umejengwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ndani ya miezi mitatu, badala ya miezi sita iliyotarajiwa tangu kutolewa agizo hilo la Rais Magufuli, Septemba mwaka jana. Katika sherehe za jana mkoani Manyara, Rais Magufuli alitangaza kuwa kuna eneo lingine limegundulika kuwa na madini hayo ya tanzanite na muda si mrefu litawekwa ukuta. Hakulitaja. Aidha, amesema hata ikibidi, Mlima Kilimanjaro utawekewa ukuta ili kuonesha msisitizo wa kulinda rasilimali za Watanzania.
“Hata ikibidi kuzungusha ukuta katika Mlima Kilimanjaro, tutafanya hivyo ili kuhifadhi rasilimali zetu,” alisema Rais Magufuli katika sherehe iliyohudhuriwa na maelfu ya watu. Mbali ya hayo, alitangaza kutoa Sh milioni 100 kwa mgunduzi wa madini hayo ya tanzanite, Mzee Jumanne Ngoma wa mkoani Kilimanjaro, ambaye kwa sasa amepooza. Alihudhuria sherehe hizo za jana akiwa na wanawe wawili. Alisema mzee huyo aligundua madini hayo mwaka 1967 na alipeleka sampuli tatu kwa mdiolojia mkuu, lakini licha ya kuvumbua madini hayo hadi leo, hakuna hata aliyemtambua badala yake wachimbaji wengine wananufaika.
Alisema mzee huyo amepooza kidogo, hivyo fedha hizo zitamsaidia kujikwamua kiuchumi na serikali inamtambua mzee huyo hadi hapo Mungu atakampomchukua. Kwa upande wake, Mzee Ngoma alimshukuru Rais kwa kumtambua na kumpatia fedha hizo akisema Rais Magufulu kuwa mtu wa watu wanyonge. Binti wa mzee huyo, Asha Ngoma alisema madini hayo awali yalikuwa yakiitwa Zoicite na baadaye kuunganishwa kuwa Tanzania kisha baadaye kuitwa tanzanite. “Tanzania hii ukifanya chochote kinachotambulika hakuna mtu anayeona thamani yako tuache roho mbaya tuwatambue wazee,” alisema Rais Magufuli na kueleza kuwa vijana 2,038 walioshiriki kujenga ukuta huo, watapewa ajira katika majeshi na kusisitiza kuwa hataki kusikia kampuni yoyote ya ulinzi ikilinda madini hayo.
Aidha, alisema Kampuni ya TanzaniteOne ilikuwa ikiibia serikali, lakini hivi sasa wapo kwenye mazungumzo ili kuhakikisha serikali inapata mapato. Alisema asilimia 40 ya madini ya tanzanite yalikuwa yakiibiwa, na kwamba kampuni 1,700 zimesajiliwa na Wizara ya Madini, lakini ni kampuni 25 tu ndizo zinalipa kodi serikalini. Alisema katika Kitalu C walifanya utafiti mwaka 2015 na kugundua kuwepo kwa tani 759 za tanzanite na tafiti hizo zimeonesha kuwa uwepo wa madini hayo hadi mwaka 2042. “Hivi unawezaje kununua ndege halafu inashikwa mnashangilia… hivi huyu mtu unawezaje kuwa naye pamoja. Huu ni utovu wa nidhamu.
Nawaomba Watanzania wenzangu bila kujali vyama, dini au kabila hebu igeni uzalendo wa vijana hawa wa Jeshi la JKT,” alieleza Rais Magufuli na kuongeza: “Tutazunguusha ukuta katika maeneo yote yenye mali na ajira za vijana hawa 2,038 zipo wazi wakuu wa majeshi kila mmoja atoe ajira kwa vijana hawa na hao maofisa wengine nitajua jinsi ya kuwapandisha vyeo na barua zao.”
Aliwaondoa hofu wachimbaji wadogo kuwa hakuna wasiwasi kuhusu ukuta, bali kunawekwa utaratibu wa kudhibiti madini hayo ili kila mtu anufaike nayo. Waziri wa Madini, Angella Kairuki alimpongeza Rais Magufuli kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania wote. Alisema umiliki na udhibiti wa rasilimali za nchi umeonesha njia na kuiweka Tanzania kama kinara wa uchumi na udhibiti wa madini. Alisema licha ya madini haya kupatikana Mirerani pekee, hayakuwa na faida kwa wananchi.
Alisema madini haya hayakutengeneza ajira nchini, bali ajira zaidi ya 30,000 zilizalishwa nchini India huku Watanzania wakiwa hawanufaiki na madini haya wala kupata ajira. Alisema wizara inaandaa Kanuni za Mirerani Control Area zitakazotoa mwongozo wa udhibiti wa madini hayo. Alisema watu 6,500 wameshasajiliwa na kuanza kupewa vitambulisho kwa ajili ya kuingia kwenye eneo hilo, na kwa kuanzia watu 10,495 wamepata vitambulisho vya Taifa na kusisitiza kuwa watu wasio na vitambulisho hawataruhusiwa kuingia eneo hilo.
Kwa mujibu wake, ndani ya ukuta huo kutakuwa na maeneo mbalimbali ikiwemo viwanda, maegesho ya magari na huduma nyingine. Hivi sasa wapo katika hatua za kufunga kamera maalumu (CCTV), mashine za skana zitakazozunguka ukuta mzima ili kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo. Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi alisema eneo hilo ni la kwanza katika historia ya uchimbaji wa madini ya tanzanite. Aliwapongeza wote walioshiriki ujenzi wa ukuta huo sanjari na makamanda wa ngazi mbalimbali wakiwemo Suma JKT sanjari na vijana wa JKT waliojitolea kujenga ukuta huo kwa haraka na mafanikio makubwa.
Alisema mahusiano mazuri yamesababisha wananchi kushirikiana na jeshi katika kulinda rasilimali za Taifa zilizopo katika eneo hilo. Alimshukuru Rais kwa imani yake kwao na alimkabidhi hati na ufunguo kama ishara ya kukamilika kwa ujenzi wa ukuta katika eneo hilo. Naye Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Martin Busungu aliwashukuru wazee wa mila na wananchi kwa kushirikiana kwa dhati kutoa historia kwenye maeneo korofi yaliyowezesha ujenzi wa ukuta huo.
Alisema jeshi lipo tayari kutekeleza maagizo yoyote atakayotoa Rais Magufuli na kusisitiza kuwa ujenzi wa ukuta huo umefanyika kwa ubora na uhakika kupitia wataalamu mbalimbali wa Jeshi na Suma JKT. Alisema ujenzi huo umeunganisha vikosi mbalimbali vya JKT na kuwatumia vijana kama nguvu kazi ya Taifa. Alisema awali gharama za ujenzi wa ukuta huo wenye urefu wa kilometa 24.5, ulikuwa ni Sh 4,862,338,398, lakini kutokana na ongezeko la kilometa 3.4, gharama zake ziliongezeka na kufikia Sh 5,645,843,163.55. Alisema ujenzi ulikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo makorongo yaliyokuwa yakijaa maji na miamba.
Pia walitumia wataalamu kutoka Bonde la Pangani ambao walitoa ushauri kwa kushirikiana na jeshi katika kutatua changamoto hizo na kusisitiza kuwa vijana wa JKT walishiriki kujenga ukuta huo. Awali, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo alisema nidhamu ya jeshi imewezesha kukamilisha ujenzi wa ukuta huo kwa muda wa miezi mitatu badala ya sita. Alisema Rais awali alipokuja kuweka jiwe la msingi Septemba, 2017 alitoa maagizo ya ujenzi wa ukuta ndani ya miezi sita, lakini agizo hilo wamelitekeleza kwa miezi mitatu ambapo Februari mwaka huu umekamilika.
Alisema waliofanikisha kujenga ukuta huo ni maofisa 34, askari 287 na vijana 2,034 kutoka vikosi viwili vya Oparesheni Magufuli na Oparesheni Kikwete waliofanya kazi kwa uzalendo na hamasa ya hali ya juu. Aliwapongeza vijana hao wanaohitaji neno la faraja kutoka kwa Rais Magufuli kwani walifanya kazi kwa moyo wa pekee bila kijali siku za sikukuu wala ugonjwa. “Nina imani Mheshimiwa Rais utatoa neno la faraja kwa vijana hawa na daima tupo imara kulinda Taifa letu na mipaka ya nchi yetu, tutaendelea kukuunga mkono na Watanzania wenzangu tujivunie Tanzania yetu na tuilinde kwani ujenzi wa ukuta huu ni ulinzi wa rasilimali zetu,” alisema Jenerali Mabeyo na kuwasisitizia Watanzania kuwa amani ni zawadi pekee tuliyonayo hivyo ni vyema kuilinda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti alisema wananchi wa Manyara wamefurahi kujengwa kwa ukuta ili kudhibiti mapato ambayo serikali ilikuwa ikiyakosa. Alisema awali wachimbaji wadogo wadogo wa madini hawakuwa wakilipa kodi, lakini hivi sasa katika kipindi cha miezi mitatu, wachimbaji hao wa tanzanite wanalipa kodi. Aidha, alisema Septemba 20, 2017 wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi kwenye Barabara ya Kia/Mererani wananchi walitoa kero zao ikiwemo ukosefu wa gari la kubeba wagonjwa na kusisitiza kuwa muda wowote gari hilo la wagonjwa litafika eneo hilo.
Kuhusu kero ya maji, Mnyeti alisema serikali imetoa Sh milioni 700.2 kutatua kero ya maji kwa wananchi hao Akizungumzia masuala ya Mkoa wa Manyara, Rais Magufuli alisema Sh bilioni 6.4 ambazo ni fedha za elimu zimetengwa, lakini pia Sh bilioni 1.9 zimetengwa kwa ajili ya Hospitali ya Mkoa wa Manyara huku akisisitiza kuwa vituo vya afya kuboreshwa ili kutoa huduma za upasuaji Alisisitiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kujenga barabara za lami, na kwamba serikali imetenga Sh milioni 100 kutengeneza barabara za lami kwenye mji huo utakaokuwa wa kisasa na maeneo mbalimbali.
Pia alikabidhi gari la wagonjwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi. Mwanzoni mwa shughuli hiyo iliyohudhuriwa na mawaziri na naibu mawaziri kadhaa, viongozi wa dini waliwaombea wachimbaji wadogo kuendelea kuchimba na kupata madini yenye manufaa kwao na kwa nchi kwa ujumla. Baada ya sala hizo vijana wa JKT walinogesha uzinduzi huo wa ukuta kwa kuimba wimbo uliowafanya wananchi na watu mbalimbali kuwashangilia. Katika kughani, waliiomba serikali kuwafikiria pale panapotokea fursa za ajira.
chama cha mapinduzi ccm mkoa wa tabora wanivunia raisi wa jamuhuli wa muungano wa tanzana

No comments