Header Ads

amwaga pongezi kwa timu YA (Ngorongoro Heroes)



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amewapongeza timu ya 
Taifa ya vijana chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na ile ya chini ya miaka 17 (Serengeti 
Boys) kwa kufanikiwa kufuzu katika michezo yao iliyochezwa jana Aprili 22, 2018 huko
 DR Congo na Burundi.

Ngorongoro Heroes wamefanikiwa kusonga kwenye raundi ya pili ya kufuzu fainali za Africa za vijana chini ya miaka 20 zitakazochezwa Niger mwezi Novemba baada ya ushindi wake wa penati 5-6 dhidi ya DR Congo baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bila kufungana kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Tanzania wakati Serengeti Boys wenyewe wamefuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Vijana ya Cecafa chini ya miaka 17 inayoendelea huko Burundi.
Rais Karia amesema kufanya vizuri kwa timu hizo za vijana ni faraja kubwa kwa Tanzania na inaonesha namna ambavyo TFF inaendelea kuwekeza kwenye soka la vijana.
"Vijana wa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys wameonesha jitihada kubwa na wanastahili pongezi kwa jitihada hizo pamoja na jitihada za mabenchi ya ufundi ya timu hizo. Tumepokea matokeo ya vijana wetu kwa furaha kubwa kwasababu tumekuwa tukihakikisha timu hizi zinapata maandalizi mazuri ambayo yanaonekana uwanjani kwa kupata matokeo mazuri ambayo yanailetea sifa kubwa Tanzania kwa ujumla", amesema Karia.
Aidha, Rais wa TFF, Karia amesema TFF itaendelea na jitihada kuzipatia maandalizi mazuri zaidi timu hizo ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali yanayowakabili.
Kwa upande mwingine, Rais Karia amewashukuru wote wanaounga mkono jitihada za TFF kuendeleza mpira wa Tanzania huku akiishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa kuunga mkono na ushirikiano wao kwa TFF.


No comments