Header Ads

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amelieleza Bunge kuwa, serikali imejipanga kuijenga Dodoma


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amelieleza Bunge kuwa, serikali imejipanga kuijenga Dodoma uwe mji bora na wa kisasa unaoendana na mahitaji na mifumo ya miji bora duniani.
Amesema, ili kutekeleza azma hiyo, Serikali inashirikiana na wadau ikiwemo sekta binafsi na mashirika ya kimataifa kuujenga mji huo.
“Natoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuendelea kuwekeza Dodoma kwani kuna fursa nyingi za uwekezaji ikizingatiwa nafasi yake kijiografia inayosaidia mikoa yote hapa nchini kufikika kwa urahisi na haraka zaidi” amesema.
Amempongeza Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua kampeni yenye lengo ya kuiwezesha Dodoma kuwa ya kijani.
Majaliwa pia ameupongeza pia Umoja wa Mataifa na mashirika yake kwa kufungua ofisi zake za muda Dodoma.
“Natoa wito kwa mashirika mengine ya kimataifa na mabalozi waige mfano huu wa kuhamishia ofisi zao Dodoma” amesema wakati anawasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2018/2019.
Amelileza Bunge kuwa, tangu Septemba 2016 watumishi wa umma 3,829 kutoka wizara na taasisi mbalimbali wamehamia Dodoma katika awamu ya kwanza na ya pili.
Amesema, ili kufanikisha azma ya kuhamia Dodoma, Serikali inaboresha miundombinu ya barabara, reli, uwanja wa ndege, umeme, mifumo ya maji safi na majitaka, ofisi, makazi na kuimarisha huduma za elimu, afya, mawasiliano na michezo.

No comments