Askofu mbaloni kwa kumuua kaka yake
JESHI la Polisi mkoani Arusha limesema linawashikilia watu watatu akiwemo Askofu Mkuu wa Kanisa la International Evangelism lililopo Sakila wilayani Arumeru mkoani hapa, Elihudi Isangya (69) kwa tuhuma za mauaji ya kaka yake.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Yusuph Ilembo amesema Askofu Isangya anashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya kaka yake, Nixon Isangya (59).
Waliokamatwa mpaka sasa kuhusika na tukio hilo la mauaji lililotokea Januari 8 mwaka jana nyumbani kwa marehemu Moivaro kwa kupigwa kichwani na kiti kizito chenye ncha kali ni pamoja na mdogo wake, Ndewario Isangya (59) na Ofisa Mwandamizi wa kanisa hilo, Obadia Nanyaro (60).
Kamanda Ilembo amewaeleza waandishi wa habair kuwa, polisi bado inamshikilia kiongozi huyo wa dini na wenzake hadi uchunguzi utakapokamilika na ikibainika kuhusika katika tukio hilo la mauaji, sheria itafuata ikiwa ni pamoja na wahusika kufikishwa mahakamani.
“Ni kweli tumemkamata Askofu Isangya na yuko rumande tangu wiki iliyopita akiwa na wenzake kwa tuhuma za mauaji na polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo,’’ alisema Kamanda Ilembo.
Habari kutoka kwa mtoto wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Jerry Nixon Isangya alisema kabla ya kuuawa kwa baba yake, baba alikuwa akiishi na kijana mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Simoni Kaaya.
Alisema mara baada ya mauaji hayo kijana huyo alitoweka lakini kwa juhudi za wananchi zilifanikisha kijana huyo kukamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi kwa upelelezi zaidi wa tukio hilo.
Mtoto huyo wa marehemu alisema kuwa baba yake alikuwa na ugomvi mkubwa na ndugu yake Askofu (yaani mdogo wake) na kufikia hatua ya kutosalimiana kwa muda mrefu, kisa wao kama watoto walikuwa hawajui.
Hata hivyo, habari ambazo gazeti hili imezipata kutoka kwa watu wa karibu wa familia ya Isangya zilisema kuwa ugomvi wa wana ndugu hao ni wafadhili wa kanisa hilo kwani marehemu ndio alikuwa mwanzilishi wa kuwasaka wafadhili hao.
Vyanzo viliendelea kusema kuwa Nixon ndiye aliyewatafuta wafadhili hao lakini inadaiwa kuwa wafadhili walikuwa wakituma fedha nyingi za ujenzi wa kanisa lakini utekelezaji wake ulikuwa sio mzuri.
Habari ziliendelea kusema kuwa Nixon aliamua kumwingiza mdogo wake, Askofu Elihudi katika kanisa hilo na kukabidhiwa baadhi ya majukumu na wafadhili walilidhika na utendaji kazi wake na kuanza kufanya naye kazi na kumtumia mamilioni ya dola ya ujenzi wa kanisa na wafadhili kuamua kubwaga marehemu na kufanya kazi na Askofu.
Vyanzo vilisema kutokana na hali hiyo ndipo ugomvi ulipoanza na vikao vya kusuluhishana vilikaa vya kifamilia lakini bila ya mafanikio na Askofu kuendelea kufanya kazi na wafadhili hao ingawa ilionekana dhahiri Nixon hakuridhika.
Post a Comment