Header Ads

Al-Shabab yauwa wanajeshi 4 wa Uganda


Somalia Al-Shabaab Kämpfer (picture alliance/AP Photo/F. A. Warsameh)
Wapiganaji wa kundi la al-Shabab lenye mafungamano na al-Qaida

Wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab la nchini Somalia wamewauwa wanajeshi wanne wa Uganda katika shambulizi kubwa dhidi ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika, katika kambi iliyo Kusini mwa Mogadishu.

Shambulizi hilo lilitokea jana Jumapili (Aprili 1) kwenye kambi iliyoko umbali wa kilomita 150 kusini mwa mji mkuu, Mogadishu.
Awali, naibu gavana wa jimbo lilikotokea shambulizi hilo, Ali Noor Mohamed, hakubainisha idadi ya waliouawa, lakini alikiri kuwa wanajeshi kadhaa wa Uganda walipoteza maisha.
Baadaye, msemaji wa jeshi la Uganda, Brigedia Richard Karemire, alithibitisha kuwa al-Shabaab imewauwa wanajeshi  wao wanne na kujeruhi wengine sita. Kundi la al-Shabaab kwa upande wake limedai kuwauwa wanajeshi 59 wa Uganda.
Pia, kundi hilo kupitia kituo chake cha redio cha Andalus limesema wapiganaji wake 14 wameuawa katika shambulizi la jana kwenye kambi ya Buula-Mareer. Msemaji wa jeshi la Uganda amesema idadi ya wanamgambo wa al-Shabab waliouawa ni 30. Umoja wa Afrika haukutoa tamko lolote kuhusu kilichotokea.
''Tumeona vifaru na magari mengine ya kijeshi ya Umoja wa Afrika yakiwa katika barabara nje ya mji wenye kambi iliyoshambuliwa'', alisema Maryam Ali ambaye ameshuhudia shambulizi hilo, na kuongeza kuwa baadaye aliweza kukimbia  yeye na watoto wake sita, kunusuru maisha yao.

No comments