Header Ads

BOHARI Kuu ya Dawa nchini (MSD) imesema kwamba magari 181


BOHARI Kuu ya Dawa nchini (MSD) imesema kwamba magari 181 yaliyozinduliwa na Rais John Magufuli mwanzoni mwa wiki yatagawanywa kulingana na ukubwa wa kanda zilizopo.
Miongoni mwa magari hayo yaliyozinduliwa na Rais Magufuli, ni LandCruiser ambayo yapo 104 na malori 77 aina ya MAN kutoka Ujerumani.
Kaimu Mkurugenzi wa Ugavi wa MSD, Byekwaso Tabura alisema jana kuwa magari hayo hayatagawanywa kwa uwiano sawa, bali yatagawanywa kulingana na ukubwa wa kanda za MSD zilizopo.
Kwa mujibu wa tovuti ya MSD, kuna jumla ya kanda nane na vituo viwili vya mauzo. Kanda hizo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Tabora, Moshi, Iringa, Dodoma na Mtwara, wakati vituo vya mauzo ni Tanga na Muleba.
Tabura amesema, Kanda ya Dar es Salaam itapata magari 21, Mwanza magari 20, Tabora na Dodoma magari 17 kila moja.
Kwa kuzingatia kigezo cha ukubwa wa kila kanda, Kaimu Mkurugenzi huyo wa Ugavi alisema kuwa kwa wastani kila kanda inaweza kupata magari 17.
“Asilimia kubwa ya madereva tunao, na kama upungufu wa madereva basi hawazidi madereva 50 kwa sababu wengine tulikuwa nao hapa na wengine wametoka kwenye baadhi ya taasisi za serikali,”alieleza Tabura.
Alisema zaidi ya magari 53 tayari yalishaanza kazi wakati mengine yakisubiri kufungwa kweye mtandao wa CarTrack ili kufuatilia mwenendo wake.
Wakati akizindua magari hayo 181, Dk Magufuli alisema kuwa magari hayo ni msaada kutoka Mfuko wa Pamoja (Global Fund) na yana thamani ya Sh bilioni 20.75 na kwamba mfuko huo wa pamoja umesaidia kupunguza changamoto ya usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini kwa kuwa hivi sasa MSD itakuwa na jumla ya magari 213 kutoka magari 32 iliyokuwa nayo awali.

No comments